Wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa jana waliungana na wenzao wa CCM kushinikiza uongozi wa Bunge kueleza sababu zilizopelekea kumkabidhi Rais John Magufuli hundi ya shilingi bilioni 6 ambazo Bunge hilo lilidai liliokoa kwa kubana matumizi, wakati bado kuna wabunge wanadai stahidi zao kwa zaidi ya miezi minne.

Siku kadhaa zilizopita, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson alimkabidhi Rais Magufuli hundi ya shilingi bilioni 6 aliyoeleza kuwa imetokana na Bunge hilo kubana matumizi.

Rais Magufuli aliagiza fedha hizo zitumike kuwapa Jeshi la Magereza ili litengeneze madawati 120,000 kwa gharama ya shilingi 50,000 kila moja, ili kila Jimbo lipate madawati 600.

Baada ya kikao cha Bunge, baadhi ya wabunge walizungumza na gazeti la The Citizen kwa masharti ya kutotajwa majina yao na kueleza kuwa pamoja na kuuhoji uongozi huo wa Bunge jana, walipewa majibu ya kisiasa ambayo hayakuwa na tija.

“Mimi nilishtuka kusikia kuwa Bunge limeweza kuokoa shilingi bilioni 6 kwa kubana matumizi na limeipa Serikali wakati mimi ni mmoja kati ya wabunge tuliokuwa kwenye Bunge lililopita na hatujalipwa mafao yetu,” alisema Mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF).

Naye mbunge wa CCM alieleza kuwa baada ya kuubana uongozi huo wa Bunge waliulizwa kuwa ‘nani hataki kupata madawati jimboni kwake’. Alisema kuwa Uongozi wa Bunge uliweka wazi kuwa fedha hizo zilipatikana kwakuwa hakukuwa na Bunge la mwezi Oktoba 2015 ambalo lilikuwa limepangiwa bajeti yake tayari.

Hata hivyo, Naibu Katibu wa Bunge John Joel alipoulizwa alieleza kuwa hakukuwa na mjadala mzito kuhusu hilo bali kulikuwa na siasa na kwamba baadae waliendelea kujadili mambo mengine ya kawaida.

RC Lindi Amtumbua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lapinga Panga la Magufuli kwenye Mishahara