Fagio la Chuma la Rais Magufuli huenda likamkumba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Za Serikali  (CAG), Profesa Mussa Assad, baada ya kudaiwa kukiuka agizo la rais John Magufuli.

Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Mtanzania zimeeleza kuwa chanzo chao cha kuaminika kutoka katika ofisi ya CAG kimeeleza kuwa alisafiri kwenda nchini Kenya Jumamosi, Disemba 12 na kurejea nchini Jumanne wiki hii bila kibali.

Imeeleza kuwa alienda nchini humo kwa lengo la kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kwamba ingawa kazi hiyo haina mahusiano na kazi ya kiofisi alitumia fedha ya umma kiasi cha shilingi milioni 15 kugharamia safari hiyo.

“Boss wetu aliondoka kwenda Nairobi Jumamosi iliyopita na kurejea Jumanne, alikwenda kutoa kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi bila kibali cha Ikulu, alipaswa kupata kibali kwa sababu ofisi yake ndio ililipa gharama,” chanzo hicho kililiambia gazeti la Mtanzania.

Hata hivyo, gazeti hilo lilipomtafuta CAG alikanusha vikali taarifa hizo na kudai kuwa hazina ukweli wowote. Alimtahadharisha mhariri wa gazeti hilo kuwa endapo watachapisha taarifa hizo atawapeleka mahakamani.

Gazeti hilo linaeleza kuwa muda mfupi baadae, Profesa Assad alimtafuta mhariri wa gazeti hilo na kumtaka kufika ofisini kwake amuoneshe kibali cha safari hiyo kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Gazeti hilo linadai kuwa mhariri wake alikuwa nje ya Dar es Salaam hivyo lilimtuma mwandishi wake. Lakini Profesa Assad alikataa kumpa mwandishi huyo nyaraka yoyote kwa madai kuwa yeye alitaka ampe mhariri ambaye alimpigia simu na sio mwandishi.

Imeelezwa kuwa baada ya mwandishi huyo kuondoka, Profesa Assad alimtumia ujumbe mhariri akimueleza kuwa hatampa tena nyaraka yoyote.

“Sitatoa nyaraka yoyote, kama unaamini chanzo chako cha habari endelea tatakutana kwa wasimamizi wenu,” unadaiwa kuwa ujumbe wa CAG kwa mhariri huyo.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipopigiwa simu ili atoe ufafanuzi alieleza kwa ujumbe kuwa alikuwa na majumu na asingeweza kupokea simu wakati huo.

Hivi karibuni, Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi wanne wa Takukuru waliosafiri kwenda nje ya nchi bila kibali.

Rais Putin aitusi Uturuki Mbele ya Waandishi Wa Habari, Amsifia Donald Trump
Dk. Kigwangalla Aweka Mtego Kuwanasa Wachelewaji Wizara ya Afya