Viongozi wa Chadema ngazi ya Taifa wamesema kuwa wamefikia uamuzi wa kufungua kesi mahakamani kudai haki ya kuuaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani Geita, Alphonce Mawazo.

Marehemu Alphonce Mawazo

Marehemu Alphonce Mawazo

Viongozi hao wamefikia uamuzi huo baada ya Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kuwazuia kuuchukua mwili katika hospitali ya Bugando na kuuaga katika ofisi za kanda za chama hicho. Polisi walieleza kuwa walichukua uamuzi huo kutokana na kuwepo hali ya hatari ya mlipuko wa kipindupindu na kwamba mikusanyiko hairuhisiwi jijini humo.

Wakiongea na waandishi wa habari jana jijini Mwanza baada ya kumaliza vikao vyao walivyokaa tangu juzi kuhusu suala hilo, viongozi hao walieleza kusikitishwa na katazo la jeshi la polisi na kwamba hawanabudi kutafuta haki ya kisheria kupitia mahakama.

“Tumeona bado tunalazimika kutafuta haki mahali pengine, na hapo pengine tunapotafuta haki ni katika mahakama. Kama chama kinachojenga demokrasia kinaamini kwamba kama tunaona hatutendewi haki na chombo chochote cha serikali basi kuna utaratibu wa kuitafuta hiyo haki katika mahakama,” alisema mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Naye waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alieleza kusikitishwa kwake na katazo la polisi huku akisisitiza kuwa hakukuwa na nia yoyote ya wananchama wa Chadema kufanya fujo mbele ya mwili wa Mawazo.

“Mimi sijawahi kuona serikali inakataza watu kuzika mtu wao. Watu hawa hawana silaha, watu hawa wanataka kumzika kwa heshima. Chadema pamoja na familia watakuwa ni watu wa mwisho kutaka kuona fujo inatokea wakati mwili wa Mawazo uko hapo,” alisema Sumaye.

Baba mzazi wa marehemu pia alieleza kuunga mkono uamuzi wa Chadema huku akilaani kitendo cha polisi kuwatawanya waombolezaji waliofika nyumbani kwake (msibani).

“Roho iliniuma kuona watu waliokuwa wamekusanyika hapo kwangu, bila kujali wametoka Shinyanga, wametoka wapi wanasambaratishwa na polisi. Nifanye nini sasa, kwa kushirikiana na Chadema kama mwenyekiti alivyosema, nikakubaliana kwamba ni bora haki ikatafutwe mahakamani,” alisema Baba Mawazo.

Alphonce Mawazo aliuwa kikatili kwa kukatwa na mapanga Mkoani Geita kwa sababu zinazoaminika kuwa ni za kisiasa.

 

 

Dk Shein aendelea Kukagua Miradi, Akagua Mji Mpya wa Kisasa Unaojengwa Zanzibar
Utata Watawala Kifo cha Ghafla Cha Msemaji Wa Madereva, Rashid Saleh