Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa kilio chao dhidi ya hoja ya kusimamisha malipo ya mshahara wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu iliyowasilishwa Bungeni.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, Tumaini Makene kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari amedai kuwa hoja hiyo ina nia ya chuki dhidi ya Mbunge huyo.
Makene alidai kuwa hoja hiyo haizingatii sheria na kanuni za Bunge kwani kuna wabunge wengi ambao wana historia za kupatiwa matibabu kwa muda mrefu huku wakiendelea kupata stahiki zao.
“Chadema tunamtaka Spika [Job Ndugai] asimamie Sheria na Kanuni za Bunge na ajue kuwa wabunge wana haki kwa mujibu wa sheria na hawafanyi kazi kwa kutegemea fadhira,” alisema Makene.
Awali, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph ‘Msukuma’ Kasheku alipendekeza Bunge kusitisha mshahara wa Lissu akieleza kuwa mbunge huyo hayuko jimboni na hayupo nchini, lakini anaonekana akiwa ‘anazurura’ katika nchi mbalimbali akiichafua taswira ya Tanzania.
Hoja hiyo iliyoungwa mkono na baadhi ya wabunge, ilimshawishi pia Spika Ndugai ambaye aliiunga mkono akieleza kuwa hajawahi kupata taarifa ya matibabu ya Lissu kutoka kwa madaktari wake kwa kipindi chote. Spika Ndugai aliahidi kuwa atafanya lile ambalo liko ndani ya uwezo wake.
Spika Ndugai alieleza kuwa Lissu alikuwa hospitali kwa muda mrefu na Bunge lilitumia busara kuendelea kumlipa ingawa hakuwa amewasilisha taarifa ya maendeleo ya matibabu yake, lakini sasa wanamuona akiwa anazunguka nchi mbalimbali badala ya kurejea jimboni kwake.
Siku kadhaa zilizopita, Spika Ndugai alieleza kuwa tangu Lissu alipoanza matibabu nchini Nairobi na baadaye nchini Ubelgiji kutokana na kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017, Bunge limeshamlipa jumla ya Sh250 milioni, ikiwa ni stahiki zake pamoja na mchango wa wabunge.
Lissu amekuwa akifanya ziara katika nchi za Ulaya na Marekani na kufanya mahojiano na vyombo vya habari pamoja na kushiriki midahalo kwenye taasisi mbalimbali.