Wakati wanachama wa klabu ya Yanga kesho wakitaraji kupiga kura katika uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya watakaoiongoza klabu hiyo kwa kipindi kingine cha miaka minne,chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA kimewatahadharisha wanachama kuwa watulivu na kupiga kura kwa amani.

Ushauri huo umetolewa na mwenyekiti wa DRFA,Almas Kasongo,ambapo amesema kwakuwa Yanga ni klabu kubwa yenye wanachama na mashabiki wengi nchini, wapiga kura hawana budi kuzingatia kuwa hali ya utulivu inatawala katika zoezi hilo kuhimu kwa mustakabali wa klabu yao.

Amewashauri pia wapiga kura kufanya uamuzi sahihi wa kuchagua viongozi wanaowaona wanafaa ili kuendeleza hali ya utulivu iliyopo kwenye klabu hiyo ambayo ndiyo mabingwa wa ligi kuu na kombe la shirikisho.

Amesema kama wanachama watashawishika na kujikuta wanashindwa kudhibiti hisia zao kwa kuleta vurugu,basi hali hiyo inaweza kuwaingia katika mfarakano mkubwa unaoweza kuharibu hata mipango yao katika michuano ya kimataifa ambapo Yanga imefanikiwa kutinga katika hatua ya makundi.

Kasongo amewahakikishia wana Yanga kuwa chama chake kipo tayari kufanya kazi kwa karibu na viongozi watakaochaguliwa ili kuendelea kuufanya mkoa wa Dar es salaam kuwa mfano wa kuigwa katika maendeleo ya soka.

Yanga itafanya uchaguzi wake kesho juni 11,2016 katika ukumbi wa Diamond Jubilee uliopo jijini Dar es salaam kuanzia majira ya asubuhi.

 

IMETOLEWA NA CHAMA CHA SOKA MKOA WA DAR ES SALAAM (DRFA)

Omary Katanga,Afisa habari DRFA

 

MO Bejaia Waanza Kujihami, Wafanya Mabadiliko
Video: Sungura Kamtie Moto |Chege Feat.Kalakala & Gift