Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wanawake wote na Watanzania kwa ujumla waendelee kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na matumizi ya teknolojia katika kujenga uchumi wa kidijitali.
Majaliwa ameyasema hayo, wakati akizungumza na wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Tano wa Mwanamke Kiongozi kwa mwaka 2023 uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa mabadiliko ya kidigitali ni moja ya vipaumbele vya Taifa kwani maendeleo ya uchumi yanategemea utandawazi..
Amesema, “nitoe rai kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kiendelee kutoa mafunzo haya ya uongozi kwa wanawake ihakikishe usawa wa kijinsia unafikiwa maeneo ya kazi, pia katika mabadiliko haya ni muhimu kutambua mchango wa wanawake katika uchumi wetu na kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya uchumi wa kidijitali.”
Aidha ameongeza kuwa, Serikali kwa kutambua umuhimu wa uchumi wa kidijitali, imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ambayo itaiwezesha nchi kutumia vema fursa za kiteknolojia zilizopo katika kuinua uchumi.
“Tayari Mkakati wa Taifa wa Brodibandi wa Mwaka 2021–2025 ambao utawezesha asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za intaneti yenye kasi ifikapo mwaka 2025 umeshaandaliwa. Serikali inaendelea na maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidigitali ili kuhakikisha nchi yetu haibaki nyuma katika ulimwengu wa kidijitali,” amesema.