Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika, limeunga mkono uzinduzi uliofanywa na ubia wa chanjo duniani, GAVI wa fursa kwa nchi kuwasilisha maombi ya fedha ili kuanza kusambaza chanjo dhidi ya Malaria.
Kupitia hatua hiyo, WHO imesema itawezesha chanjo hiyo kufikia watoto walio hatarini zaidi kwa kuanzia na Ghana, Kenya na Malawi, ambazo tayari zilianza majaribio ya chanjo hiyo mwaka 2019 na hatimaye kusambazwa nchi zingine ambako Malaria imekuwa ni sugu.
Taarifa ya WHO, Kanda ya Afrika iliyotolewa leo mjini Brazaville Congo imesema, Malaria inasalia kuwa sababu kuu ya magonjwa na vifo miongoni mwa watoto katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.
Usaidizi huo wa kimataifa utatenga dola milioni 160 kati ya mwaka huu wa 2022 hadi 2025 ili kuwezesha ongezeko la upatikanaji wa chanjo ya Malaria kwenye maeneo hatarishi zaidi Afrika.
Mkurugenzi wa WHO, kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema, “fungu jipya la fedha kutoka GAVI linatusogeza hatua mbele zaidi kukaribia mamilioni ya watoto barani Afrika na chanjo hiyo ya Malaria , RTS, S.
Wakati wa janga la Uviko-19, pindi vituo vya huduma za afya vilipokumbwa na changamoto, wazazi na walezi waliendelea kwa umakini kupeleka watoto wao ili wapate chanjo dhidi ya Malaria kutokana na wengi wa kufariki kila siku kwa ugonjwa wa Malaria na wako makini kulinda watoto wao dhidi ya ugonjwa huo.
Kufuatia pendekezo hilo la mwezi Oktoba mwaka 2021, juu ya kusambaza matumizi ya chanjo ya Malaria, miongoni mwa watoto katika maeneo ambako maambukizi yameshamiri, mataifa mengi ambako Malaria imejikita, yaliwasilisha ombi la kupata chanjo hiyo na WHO inasema itawasilisha rasmi maombi huko GAVI.
Chanjo hii ya Malaria aina ya RTS, S inazuia vimelea vya Malaria aina ya Plasmodium Falciparum, kimelea ambacho ni hatari zaidi na kinapatikana zaidi barani Afrika katika maeneo ambayo chanjo hiyo imeanza kutolewa na ambako kuna upungufu mkubwa wa idadi ya watoto wanaokwenda hospitali kwa kuugua Malaria na kupelekea vifo.
GAVI imedokeza kuwa muda wa mwisho wa maombi ya awali ya kupatiwa msaada huo ambao ni mwezi Septemba mwaka huu wa 2022 ni kwa nchi ambazo tayari zinatumia chanjo hiyo.
Dirisha la pili la maombi lililo wazi kwa mataifa mengine yanayokidhi vigezo litafungwa mwezi Januari mwaka 2023, ambapo kwa mwaka 2020 takribani watoto laki 5 barani Afrika walikufa kwa Malaria. Mtoto mmoja hufariki dunia kila dakika moja kwenye eneo la Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara.