Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga (62) amesema hatasau akikumbuka jinsi alivyovuliwa nafasi ya Uwaziri mwaka 2016 kwa madai kuwa alilewa, wakati siku ya tukio alikuwa anaumwa na alitumia dawa.

Kitwanga, ameyasema hayo, katika mahojiano maalum na Mwandishi wa kituo hiki, na kudai kuwa mambo hayo hutokea katika siasa, ambapo waweza kutengenezewa zengwe, kulongwa au kumalizwa.

Amesema, “Wakati huo nilikuwa naumwa sana, nilikuwa nakunywa dawa, huwa sitaki sana kukizungumzia kitu hicho huwa kinaniumiza sana, kwa sababu nilijua, ninajua na wenyewe wanajua walichofanya, ila hayo yamepita kwa sababu ndio maana nasema tumshukuru Mungu kwa kila jambo.”

Mwanasiasa, Charles Kitwanga.

Mwanasiasa huyo, alikuwa akinukuu maneno ya Balozi Humphrey Polepole ambaye awali pia alifanya mahojiano maalum ndani ya studio za Dar24 alipokuwa akizungumzia mambo ya siasa, ambapo alisema katika siasa yapo mambo hayo matatu ya zengwe, kulogwa au kumalizwa.

Kuhusu madai ya kurogwa Kitwanga amesema, “Nilipata kiharusi, nikalazwa Muhimbili nikaenda kupona India, nadhani nilipona kimiujiza kwa kuwa namuamini Mungu, kuwa hali uliyonayo sasahivi si maamuzi yako, bali maamuzi ya Mwenyezi mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye amekufikisha hapo.”

Aidha amefafanua kuwa, “Huwa inaniumiza nikikumbuka jinsi nilivyovuliwa uwaziri, kwani nilijua, ninajua na wenyewe wanajua walichofanya maana wakati nawania Ubunge 2020 nilikuwa nafuatiliwa kila ninakokwenda.”

Charles Kitwanga (kushoto), akihojiana na Mwandishi wa Dar24, Stanlaus Lambart, Kulia ni Humphrey Edward.

Amefafanua kuwa, “Kulikuwa na magari mawili kwa siku kumi, ndani ya magari hayo kulikuwa na vijana wa PCCB, Usalama wa Taifa na Askari, ni kama ilikuwa mashindano ya Kitwanga na Serikali lakini John Magufuli alikuwa ni rafiki yangu.”

Kuhusu suala la kuingia Bungeni huku akiwa amelewa, Kitwanga amesema,
“Pombe gani ambayo inifanye niingie nimelewa, Miaka mitano nilikua naibu Waziri, na siku zingine nilikua najibu maswali ya wizara zaidi ya tatu, leo hii nikiwa ‘Full Minister’ ndio niingie nimelewa? Ni uzembe wa namna gani huo?”

Hata hivyo amesisitiza kuwa, “Ni lazima utambue unaishi mara moja na dakika moja ikipita hairudi, kwa hivyo lazima ufurahie wakati uliopo huku akisisitiza kujituma katika kazi kwa uadilifu na Mungu atafanya mengi katika siku zako uwapo Duniani.”

Malkia Elizabeth II afariki akiwa na miaka 96
Barakoa si lazima:Ummy Mwalimu