Mabingwa wa soka nchini England, klabu ya Chelsea, usiku wa kuamkia hii leo walishindwa kujipapatua kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, hatua ya 16 bora, pale walipokutana na mabingwa wa soka kutoka nchini Ufaransa, Paris Saint Germain kwenye uwanja wa Stamford Bridge jijini London.

Chelsea, ambao walikua nyuma kwa mabao mawili kwa moja kabla ya kipyenga cha mwanzo cha mchezo huo hakijapulizwa, walitarajiwa huenda wangelipiza kisasi cha kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza, lakini mambo hayakua hivyo na badala yake walijikuta wakiendeleza uteja mbele ya PSG.

Mabao ya Paris Saint Germain, katika mchezo huo yalipachikwa kimiani na Adrien Rabiot, kwenye dakika ya 16 huku Zlatan Ibrahimovic akifunga la pili katika dakika ya 67 na Diego Costa aliifuta machozi The Blues kwa kufunga bao dakika ya 27

Kwa mantiki hiyo sasa Chelsea wametupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao manne kwa mawili, na sasa wanaungana na AS Roma pamoja na KAA Gent ambao walishindwa kufuzu katika hatua ya robo fainali kufuatia kubanjuliwa kwenye michezo yao siku mbili zilizopita.

Wakati huo huo klabu ya Zenit St. Petersburg ya nchini Urusi, nayo imeshindwa kufurukuta mbele ya Benfica kutoka nchini Ureno baada ya kufungwa mabao mawili kwa moja usiku wa kuamkia hii leo.

Zenit St. Petersburg wametupwa nje ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, hatua ya 16 bora, kwa kukubali kufungwa jumla ya mabao matatu kwa moja, kufuatia mchezo wa mkondo wa kwanza kukubali kufungwa bao moja kwa sifuri.

Zoezi La Kusaka Suluhu Lashindikana
Polisi Zanzibar Yatamba Kutetea Taji Lao Uganda