Chui-milia, kwa lugha ya kigeni ‘tiger’ wa hifadhi ya wanyama ya Bronx, New York, Marekani amekuwa mnyama wa kwanza anayehifadhiwa na Serikali kukutwa na virusi vipya vya corona (covid-19).

Mnyama huyo anayeitwa Nadia mwenye umri wa miaka minne, alipimwa baada ya kuonesha dalili za kuwa na kikohozi kikavu. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hifadhi hiyo, kuwa mnyama huyo anaendelea vizuri.

Sampuli ya Nadia ilichukuliwa pamoja na sampuli za chui-milia wengine watano na simba kadhaa ndani ya hifadhi hiyo, wote walianza kuonesha dalili za kuwa na dalili za tatizo kwenye mfumo wa upumuaji.

Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA) imeeleza kuwa hakuna wanyama wengine ndani ya hifadhi hiyo walioonesha dalili hizo.

“Ingawa wengi wameonesha dalili za kupunguza hamu ya kula, chui na simba kwenye hifadhi ya Bronx wanaendelea vizuri na wako chini ya uangalizi makini,” imeeleza taarifa ya USDA.

Dkt. Paul Calle wa hifadhi hiyo, amesema kuwa vipimo vya Nadia vilifanywa katika maabara maalum ambayo ni tofauti kidogo na ya vipimo vya binadamu.

Mamlaka ya Hifadhi hiyo imeeleza kuwa wanyama hao waliambukizwa na wafanyakazi wa hifadhi hiyo ambao walikuwa wameathirika na virusi vya corona. Hifadhi hiyo ilifungwa tangu Machi 16, 2020.

Marekani ndilo taifa linaloongoza hivi sasa kwa visa vingi vya virusi vya corona, ambapo zaidi ya watu laki tatu (300,000) wameripotiwa kupata virusi hivyo na watu 8,100 wamepoteza maisha.

Aliyemng’oa Gadaffi madarakani afariki kwa corona
Makonda kuwakamata wanaozurura mjini kuepuka corona