Chuo cha Ustawi wa Jamii, kimetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa malezi na makuzi ya watoto zaidi ya kwa wasichana 100 ambao wanaofanya kazi za ndani katika Mkoa wa Dar Es Salaam, baada ya kuona umuhimu kutokana na mchango wao na kukaa na watoto kwa muda mrefu.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Joyce Nyoni amesema, “tumeona muitikio wa wadada kuja katika mafunzo haya, lakini maombi yaliyotufikia ni zaidi ya 200 hivyo watafanya mafunzo hayo zaidi siku zijazo na leo tuna programu ya kuwajengea uwezo wadada wakazi katika malezi na makuzi ya mtoto tumeifanya hili tukiwa tunaelekea kuadhimisha siku ya ustawi wa Jamii Machi 21.”
Amesema, akinamama wengi wanaondoka asubuhi na kurudi jioni na wengi wa kina dada wamekuwa hawana uelewa kuhusu malezi na makuzi na ana mchango mkubwa katika kulea na kwamba baada ya kutoa tangazo hilo watu wengi walihamasisha kupata haki zao, kitu ambacho kinaonesha kuwa hawakai nao vizuri.
“Lakini tunatambua dada huyu kuna siku atakuwa mama ni muhimu kuelewa ni namna gani anapaswa kulea mtoto kutokana na mabadiliko tunamjenge uwezo wa kumuelewa mtoto na kuwa na msaada chanya katika maendeleo na makuzi ya mtoto,”amesisitiza.
Aidha ameongeza kuwa, “niwasihii sana hawa ni wale ambao tunawaachia watoto tukae nao vizuri hakuna binadamu ambaye hana mapungufu aelekezwe vizuri kwasababu ndio tunawaachia watoto jinsi unavyokaa naye vibaya anaweza kuhamishia kwa watoto wananafasi kubwa sana katika malezi na makuzi ya watoto.”
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, mmoja wa wafanya kazi wa ndani kutoka Bunguruni alisema yamewajenga uwezo kwani wanafundishwa vitu wanavyotakiwa kujua pia kama wazazi wa baadae na kusema “tumefundishwa kuhusu ukuaji wa mtoto kimwili, kiakili, kiroho na kijamii.”
Ameongeza kuwa, “mafunzo haya yanatujengea uelewa na hatua za ukuaji anazopitia mtoto lakini zipo changamoto tunazokutana nazo ikiwemo mahusiano ya mtoto na mama kwani muda mwingine mama anakuwa bize hapati muda wakuongea kujua napitia changamoto gani, anakuwa bize na simu au anaenda chumbani kulala.”
Wahadhiri wa Chuo hicho wametoa pia mafunzo ya Jinsi ya kukabiliana na misongo ya mawazo, matumizi sahihi ya fedha na kuweka akiba, usafi na mawasiliano.