Uongozi wa klabu bingwa nchini England Leicester City, umetangaza kumtimua Claudio Ranieri baada ya kuchoshwa na mwenendo wa matokeo yanayopatikana kwa msimu huu wa 2016/17.

The Foxes wametangaza maamuzi hayo ikiwa ni baada ya miezi 9 kwa mkuu huyo wa benchi la ufundi kuiwezesha Leicester City,  kuandika historia ya kutwaa ubingwa wake wa kwanza tangu ilipoanzishwa mwaka 1884.

Taarifa iliyotolewa kwenye tovuti ya klabu hiyo imeeleza kuwa, meneja huyo kutoka nchini Italia, amesitishiwa mkataba wake baada ya wajumbe wa bodi kuafiki kwa kauli moja kuhusu maazimio ya kutimuliwa kwake.

Kutimuliwa kwa Ranieri mwenye umri wa miaka 65 kumekuja baada ya saa 24 zilizoshuhudia kikosi chake kikipokea kisago cha mabao mawili kwa moja dhidi ya Seville CF, kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Msimu uliopita Leicester City walitwaa ubingwa kwa zaidi ya point kumi dhidi ya Arsenal waliomaliza katika nafasi ya pili, lakini msimu huu, wameshacheza michezo 25 na kushinda mitano pekee, huku ikisalia michezo 13.

Leicester City kwa sasa inashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka nchini England, na endapo itapoteza point moja itaingia katika shimo la timu zitakazofikiriwa kushuka daraja mwishoni mwa msimu.

Endapo itatokea Leicester City wanashuka daraja, wataandika historia mpya katika ligi ya nchini England ya kuwa bingwa aliyeshindwa kutetea taji lake na kuporomoka hadi ligi daraja la kwanza.

Kwa mara ya mwisho tukio hilo lililotokea mwaka 1938 ambapo Man City walishindwa kutetea ubingwa wao na kujikuta wakishuka daraja kutoka ligi daraja la kwanza hadi la pili.

Trump atangaza kujenga kinu kikubwa cha silaha za nyuklia Marekani
Magazeti ya Tanzania leo Februari 24, 2017