Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Godigodi amelazimika kutumia usafiri wa trekta kwenda umbali wa Kilometa 60 kutoka Ifakara mjini, ili kuwafikia wananchi wa Kijiji cha Chiwachiwa kilichopo Kata ya Mbingu, wilayani Mlimba kutokana na ubovu wa Barabara.
Wilaya hiyo iliyopo Mkoani Morogoro inakabiliwa na ubovu wa miundombinu kwa baadhi ya maeneo ambapo Godigodi amesema alilazimika kufika eneo hilo kutokana na utaratibu aliojiwekea wa kutatua kero za wananchi hasa wale wanaoishi pembezoni.
“Nikiwa msaidizi wa Rais Samia Suluhu Hassan nina wajibu wa kutatua na kusikiliza kero za wananchi hivyo nimeweza kusafiri kwa kilometa 60 kutoka Ifakara mjini ili kifika kwa wananchi wa Kijiji cha Chiwachiwa lengo ni kutatua kero za Wananchi,” amesema Godigodi.
Pamoja na hatua hiyo pia Mkuu huyo wa Wilaya amesema, kupitia bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2022/2023 tayari wametenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Barabara hiyo.