Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutumia Mitambo ya uchimbaji visima ilionunuliwa na serikali kwa matumizi yaliokusudiwa ikiwemo kutoa huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu na kuacha tabia ya kuzoea matatizo ya Wananchi bali wayatatue kwa weledi.

Dkt. Mpango amesema hayo wakati akikagua magari na mitambo ya uchimbaji visima na mabwawa yaliokabidhiwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2021/2022 iliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam leo Machi 20, 2023.

Amesema, serikali inaendelea kutafuta njia bora na fupi zaidi katika utoaji wa msamaha wa kodi ili kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo miradi ya maji na kukemea mitambo hiyo kutumika kwa matumizi binafsi, huku akiiagiza RUWASA kutoa huduma zaidi kwa wananchi kuliko kufanya biashara.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akizindua Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2021/2022 iliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam leo tarehe 20 Machi 2023. (Kushoto ni Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Prof. Mark Mwandosya.

Aidha, Makamu wa Rais pia ameagiza kufanyika tathmini ya bei zinazotumika na RUWASA kuchimba visima binafsi vya wananchi ili kuhakikisha haziwi juu zaidi ya bei za kampuni binafsi na kuwataka kuacha kuzoea matatizo ya wateja na hivyo kutotimiza majukumu yao kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuongeza nguvu katika kufanya ukaguzi wa ankara za maji zinatolewa kwa wateja wa Mamlaka za Maji zote nchini na zile zitakazobainika kukiuka utaratibu uliowekwa zishughulikiwe kwa mujibu wa taratibu ikiwemo mamlaka zote za maji ambazo zinatoza bei ambazo hazijaidhinishwa na EWURA.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema matokeo yaliopatikana kwenye sekta ya maji kutokana na udhibiti unaofanywa na EWURA kwa mamlaka za maji ni pamoja na kuhakikisha mamlaka za maji zinaandaa mipango ya biashara ambayo inawawezesha kupata bei za maji.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akitoa maelekezo kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira
Vijijini (RUWASA)juu ya matumizi sahihi ya mitambo maalum ya uchimbaji visima wakati wa ukaguzi wa mitambo hiyo katika hafla ya Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2021/2022 iliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam leo tarehe 20 Machi 2023.

Amesema baadhi ya mamlaka za maji zimepunguza utegemezi kwa serikali kwa kulipia gharama za uendeshaji na kutumia mapato ya ndani na mikopo kutekeleza miradi mikubwa ya maji ya kuongeza upatikanaji wa majisafi katika maeneo ya miji wanayoisimamia.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile amesema lengo la uzinduzi wa taarifa hiyo ni kuibua changamoto zilizopo katika mamlaka za maji na kuwezesha serikali na wadau mbalimbali kuona maeneo ya vipaumbele vya uwekezaji na kuandaa mipango ya kuboresha utoaji huduma za majisafi na usafi wa mazingira.

Dkt. Andilile amesema EWURA itaendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha taifa linakuwa na huduma za maji za kutosha zenye uhakika katika hali endelevu kwa kuhamasisha na kusimamia ufanisi katika utendaji kazi wa mamlaka za maji.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 21, 2023
TPLB yampongeza Rais Samia Suluhu