Kwa sisi wazazi tunafahamu… ukiona mtoto anakusalimia zaidi ya mara mbili asubuhi tena kwa msisitizo, basi ujue kuna ombi lake nyuma ya hizo salamu, na huenda likawa ombi zito na anatafuta tu ‘gia’ ya kuanzia.
Basi nianze kwa kuweka wazi mtazamo wangu kuwa kinachoitwa bifu kati ya Diamond na Ali Kiba, sioni kama ni sehemu ya vipaumbele vya kitaifa bali ni uhasimu wa muziki unaochochea biashara. Utanielewa ukiendelea..!
‘Awali ya yote’ (kihenga), nampongeza kwa moyo wa dhati Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo adhimu ya kufanya kazi na kiwanda ambacho kwanza ni mdomo wa jamii (habari) lakini pia ni chanzo cha furaha na kipato (sanaa na utamaduni).
Ingawa Dkt. Mwakyembe amekabidhiwa ofisi ikiwa na changamoto nzito ya mengi yaliyojili kabla na baada ya mtangulizi wake, Nape Nnauye (Mbunge wa Mtama) kuondolewa katika nafasi hiyo, naweza kusema ametua kwenye ardhi akiwa tayari anakimbia. Waingereza husema ‘You hit the ground running’.
Kwa muda mfupi ameanza kuyashughulikia baadhi ya mambo ukipokea kijiti kutoka kwa Nape ambaye kwa hakika alifanya kazi nzuri iliyokubalika. Na hata wakati anaondoka dalili zilionesha jinsi tasnia ilivyompenda, ingawa alikuwa na mapungufu yake pia kama binadamu na kiongozi.
Nampongeza Mheshimiwa Mwakyembe kwa kulivaa vyema suala la kuiwezesha Serengeti Boys na safari yake ya ‘Gabon mpaka Kombe la Dunia’.
Lakini pia ni namna alivyoweka wazi mpango wako wa kuwapatanisha Diamond na Alikiba, ambao ni mahasimu wa kimuziki na mafahari wawili kwenye zizi la Bongo Fleva.
Ingawa kiuhalisia uhasimu huu wa kibiashara unaweza usiwe ‘suala la kitaifa’, na huenda ndio unaowatengenezea biashara zaidi kati yao ndani ya nchi, nataka kusema kama amethubutu kutaka ‘kuutafuta’ mfupa huu, naomba utusaidie sisi wasanii na wanahabari kuutafuta huu mfupa alioanza nao Mheshimiwa Nape lakini ukaingia kwenye mkanganyiko mzito. Nguvu kubwa aelekeze huku.
Nadhani huu ndio mfupa muhimu zaidi, weka kando uhasimu wa kibiashara wa Diamond na Ali Kiba ambao baadhi ya watu wamewahi kusikika wakitamani kuufanyia biashara kubwa zaidi uhasimu huu kwa kuuchochea na kufanya tamasha kubwa zaidi.
Mfupa huu ninaoutaja, ni mpango wa wasanii kuanza kulipwa fedha kwa nyimbo zao kuchezwa katika vituo vya runinga na redio, suala ambalo mtangulizi wake Nape Nnauye alilitangaza kuanza rasmi Januari Mosi mwaka jana, lakini likagonga mwamba hadi leo huku mjadala ukionekana kama vile umefungwa.
Nayakumbuka maneno ya Nape, Desemba mwaka jana yakiwa na nia ya dhati baada ya kueleza wazi kuwa mtambo wa kung’amua nyimbo za wasanii zilivyopigwa kwenye vituo vyote vya runinga na redio uko tayari na kampuni ya CMEA ndiyo iliyokuwa na jukumu hilo.
“Tumeamua kuanza kuyafanya haya kwa vitendo, kwamba kuanzia tarehe 1 Januari mwaka 2016 kituo chochote cha redio na televisheni kikipiga wimbo wa mwanamuziki basi kitatakiwa kumlipa yule mwanamuziki,” alisema Nape kabla ya kutoa mchanganuo wa namba vituo hivyo vitakavyotoa asilimia 30 ya faida ya matangazo yake na kuikabidhi COSOTA ambayo itawasilisha kwa wahusika.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya neema iligeuka kuwa shubiri na kupingwa na wasanii wengi ambao walitakiwa kuneemeka.
Moja kati ya vikwazo vilivyowekwa na wasanii hao ni kuipinga kampuni ya CMEA iliyopewa jukumu hilo, kwa madai kuwa ni kampuni inayomilikiwa na PushMobile ambayo wao walidai wanahistoria mbaya ya kufanya nayo kazi kwenye biashara ya miito ya simu.
Kikwazo kingine kilichowekwa na wasanii ni kuhusu muundo na utendaji kazi wa COSOTA, wakidai kuwa kwa mujibu wa sheria iliyoianzisha, inapaswa kuundwa na kusimamiwa na wasanii wenyewe na kwamba hali haiko hivyo. Pia, walikosoa utendaji wake wakidai kuwa hawatekelezi majukumu yao ikiwa ni pamoja na jukumu dogo la kuwashauri wasanii. Hivyo, hawana imani nayo.
Kutokana na sintofahamu hiyo, ni mwaka mmoja sasa umepita na bado kuna wingu zito limetanda isijulikane ni nini hasa kinapaswa kufanyika ili mpango huo uende kama ulivyokusudiwa bila kuumiza upande wowote.
Lakini pia, namna bora ya kuwaokoa wasanii wanaochipukia wasifukiwe na mpango huo kwani kwa sasa wao ndio hulazimika hata kuwapooza kwa chochote watangazaji ili nyimbo zao zipate nafasi .
Kwa namna ninavyouamini utendaji wa Waziri Mwakyembe katika wizara mbalimbali ulizowahi kushika na kamati nzito ulizowahi kuziongoza kwa masuala nyeti ya kitaifa, ninaamini akiubeba mfupa huu, atautafuna vilivyo na tutapata matokeo chanya yaliyokusudiwa.
Tukumbuke kuwa wasanii wetu kama Diamond na Rose Mhando, hulipwa miamala mikubwa kwa kazi zao kuchezwa kwenye vituo vya nchi mbalimbali. Hivi karibuni, Rose Mhando alitajwa kuwa ndiye Mtanzania anayepokea kiasi kikubwa cha fedha kutoka nje ya nchi kwa kazi zake kutumika kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchezwa kwenye vituo vya redio na runinga.
Simpangii! Namshauri Waziri Mwakyembe kulishikia bango suala hili kwani ni muhimu kuliko ‘tension’ iliyopo kati ya Diamond na Ali Kiba. Hawa wanaweza kupatanishwa tu siku moja na wadau wa muziki au hata wao wenyewe kama ilivyokuwa kwa AKA na Cassper Nyovest wa Afrika Kusini, ambao bifu lao lilikuwa kubwa zaidi barani Afrika.
Naamini katika masuala ya kitaifa kama kuipigia debe Serengeti Boys, ni dhahiri kuwa wawili hawa wataungana ‘kwa sababu maalum’ kama ilivyokuwa kwenye tafrija ya wasanii kumuaga Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, kwahiyo hilo naomba nimtoe hofu Waziri Mwakyembe.
Hata Marekani na ulaya, ukiweka mbali ‘gangster beef’ inayohusisha ugomvi wa kutumia silaha, uhasimu wa kimuziki na mitandaoni umekuwa chachu na humalizwa na wasanii wenyewe au kupitia wadau. Mfano mwingine ni Jay Z na Nas, 50 Cent na Fat Joe na wengine wengi.