Baada ya mgomo wa muda mrefu wa madaktari nchini Kenya uliopelekea Serikali ya nchi hiyo kuomba madaktari kutoka Tanzania, umechukua sura mpya baada ya Mahakama nchini kutoa zuio la kuajiri madaktari kutoka Tanzania.

Zuio hilo limetolewa na Mahakama hiyo huku ikisema kuwa kuna idadi kubwa ya madaktari nchini humo ambao hawana ajira hivyo hakuna haja ya kuajiri wengine kutoka nje ya nchi.

Kenya iliomba madaktari 500 kutoka Tanzania ili kupunguza uhaba waliokuwa nao baada ya kutokea mgomo wa wataalamu hao wa Afya uliodumu kwa muda mrefu.

Aidha zuio hilo la Mahakama litadumu mpaka pale suala lililosababisha mgomo huo litakapo patiwa ufumbuzi.

Akifafanua kuhusu taarifa hiyo ambayo imesambaa mitandaoni, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Vijana, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa iwapo Kenya italeta tamko la kughairi ombi walilotoa la kutaka kuajiri madaktari kutoka Tanzania Serikali itaheshimu uamuzi huo.

“Kwanza kabisa hiyo ni fursa kwa madaktari wetu kupata ajira, lakini kama ni kweli zuio hilo limetolewa, basi Serikali inasubiri tamko rasmi litakapopokelewa na tutasitisha zoezi la kuandikisha madaktari walioitikia wito huo ambao ni mkubwa,”amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo waraka huo wa zuio umetoa siku 21 kwa Serikali ya Kenya kutoa majibu ya malalamiko yaliyopelekwa na mahakamani na madaktari wa nchi hiyo.

 

Makala: Mwakyembe Tusaidie Kuutafuna Mfupa huu, Ni Zaidi ya Bifu ya Diamond na Ali Kiba
Video: Zitto, Chedema watifuana tena, Serikali yalainika hoja Katiba mpya