Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula amewafunda Wakuu wa Ukaguzi wa Ndani na Wahasibu Wakuu wa Wizara hiyo na taasisi zake ikiwemo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Baraza la Watumiaji wa Huudma za Mawasiliano Tanzania (TCRA. – CCC), Tume ya TEHAMA (ICTC) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wakati akifungua kikao kazi hicho kilichofanyika Dodoma.
Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Wakaguzi Wakuu wa Ndani ni jichola taasisi, ni wasomi, watalaam wa kufanya ukaguzi na kubaini hoja zilizopo ndani ya taasisi hizo na wanawajibika kumshauri mkuu wa taasisi mapema na kwa wakati ili hoja hizo zifanyiwe kazi mapema na kwa wakati na zifungwe ndani ya muda wa mwaka wa fedha husika.
Amesisitiza kuwa, “tusisubiri mpaka mgeni aingie ndiyo uanze kusafisha nyumba maana utaacha buibui,” amesema Chaula na kuongeza kuwa ni muhimu kwa Wizara na taasisi zake kupata hati safi badala ya kupata hati chafu au yenye mashaka kutoka Ofisi ya CAG kwa kuwa wao wapo ndani ya taasisi, wanafahamu yanayotekelezwa na taasisi zao na muda wa ukaguzi unajulikana hivyo amewataka wajipange mapema na kuandaa nyaraka za ukaguzi badala ya kusubiri wakaguzi wa Ofisi ya CAG kuibua hoja za ukaguzi.
Amewataka wataalam hao kuhakikisha kuwa mipango, mapato na matumizi yanaendana na wakumbuke kuwa Wizara hii ni ya TEHAMA, hivyo wahakikishe wanakwenda na kasi ya ukuaji wa TEHAMA na taratibu za ukaguzi kwa kuwa TEHAMA ni msingi wa maendeleo.
Muandaaji wa kikao kazi hicho, Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani wa Wizara hiyo, CPA.Joyce Christopher amesema kuwa malengo ya kikao hicho ni kuhakikisha wataalam hao wanakuwa na uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu ili kuhakikisha kuwa thamani ya fedha ya miradi ya maendeleo na majukumu yanayotekelezwa na taasisi hizo inapatikana ili Serikali iweze kuhudumia wananchi wake.
Akizungumza kwa niaba ya wataalam hao, Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani wa TTCL, CPA. Octavian Barnabas amesema kuwa anaishukuru Wizara kwa kuandaa kikao kazi hicho ili waweze kuwa na uelewa wa pamoja ya kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao.
Wataalam hao watakuwa na ajenda nyingine kwenye kikao kazi hicho ikiwa ni pamoja na kujadiliana kuhusu hoja za CAG za mwaka wa fedha 2019/2020; utekelezaji wa mapendekezo ya CAG kwa mwaka wa fedha 2019/2020; ushiriki wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani katika ufungaji wa hesabu na ukaguzi wa CAG; na uandaaji wa hesabu za mwaka wa fedha 2020/2021.