Kiungo mahiri wa Mbeya City FC, Ayoub Semtawa atalazimika  kusubiri kwa majuma mawili zaidi ili kuweza kurejea  uwanjani, kufutia majeraha ya kuchanika nyama za paja la mguu wake wa kulia kwenye mchezo dhidi ya African Lyon  uliochezwa jijini Dar,wiki moja iliyopita.

Kwa mujibu wa daktari wa kikosi, Dr Selaphini Mushi, Semtawa  alichanika  vibaya nyama za paja baada ya kugongwa na mlinzi wa Lyon wakati alipokuwa akijaribu kumiliki mpira wa juu na kulazimika kutolewa  nje kwa msaada baada  kushindwa kabisa kutembea, kufuatia tukio hilo lililotokea  katika dakika ya 60 ya mchezo huo.

“Baada ya kutolewa ilitulazimu kumpa magongo ili aweze kutembea kwa sababu alikuwa hawezi, juma moja limepita sasa ameacha kutumia magongo na anaweza kutembea mwenyewe, taratibu za matibabu zinaendelea lakini atalazimika kusubiri wiki mbili zaidi ili kuweza kurejea kwenye hali yake ya kawaida na hatimaye kurejea tena uwanjani, hatuna shaka sana na hali yake kwa sasa nina imani kubwa baada ya muda huo atakuwa tayari kwa kuitumikia timu” alisema.

Katika hatua nyingine Dr Mushi alithibitisha kupona na kuanza mazoezi kwa mlinda mlango Owen Chaima  ambaye alitolewa nje kwenye mchezo uliopita dhidi ya Majimaji kufutia maumivu makali  ya mgongo aliyopata  wakati akiwa kwenye majukumu.

“Chaima alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Fikirini Bakari, alipata maumivu makali wakati akiwa kwenye mchezo, jambo jema ni kuwa baada ya matibabu sasa yuko fiti kabisa  na amefanya mazoezi siku ya jana na leo atafanya pia kwa ajili ya kujiweka sawa tayari kwa mchezo dhidi ya Yanga hapo kesho kama ilivyo kwa mshambuliaji Geofrey Mlawa ambaye naye aliumia lakini sasa yuko kwenye hali nzuri kabisa” aliongeza Dr. Mushi.

Kinnah Phiri: Tupo Tayari Kuwakabili Young Africans
Mustakabali Wa Frank de Boer Bado Ni Kizungumkuti