Kocha mkuu wa Mbeya City  FC, Kinnah Phiri amesema ameajindaa vizuri  ‘kuikabili’ Young Africans  kwenye mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara uliopangwa kuchezwa kesho jumatano kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Muda mfupi uliopita Kocha Phiri ameiambia tovuti ya klabu hiyo ya jijini Mbeya na kusema anaamini utakuwa mchezo mzuri na mgumu kwa sababu timu zote mbili zimetoka kushinda michezo iliyopita huku akiahidi ‘kuiduwaza’ Yanga kwa kipigo kutokana na maandalizi  mazuri aliyoyafanya kwa kikosi chache na kutupilia mbali hofu yoyote kutoka kwa timu hiyo, akiamaini timu zote hizi mbili zina mchezo sawa.

“Kweli, kesho tunacheza na Yanga, utakuwa mchezo mzuri kwa sababu timu zote zimeshinda michezo iliyopita,sisi tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda,hatuna shaka yoyote kwa sababu timu zote zina mchezo sawa, jambo jema ni maandalizi tuliyoyafanya na sapoti ambayo tutaipata kutoka kwa mashabiki wetu, watu waje uwanjani na wajiandae kushangaa kile kitakachofanywa na timu yangu”alisema.

Akiendelea zaidi kocha huyo raia wa Malawi alisema kuwa City imebakiza michezo miwili, wa kesho na ule wa tarehe 7 dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Manungu Turiani,  hivyo anachokitizama sasa ni kushinda michezo hii miwili ili kuweza kupata pointi 6 ambazo  zitaiwezesha timu yake kufikia nafasi  nzuri kwenye msimamo wa ligi kabla ya kukamilika kwa duru ya kwanza.

“Tumebakiwa na michezo miwili, wa kesho na ule ambao tutacheza dhidi ya Mtibwa, tuko kwenye nafasi ya tisa sasa, lengo letu ni kushinda michezo hii ili kuweka mazingira mazuri katika msimamo wa ligi kabla hatujamaliza duru la kwanza, hii ina maana kuwa tutakaporejea kuanza duru ya pili tutacheza kwa nguvu kutafuta nafasi mbili za juu.” Aliongeza Phiri.

ZIFA Waialika Taifa Stars Mjini Harare
Dr Mushi: Semtawa Atasubiri Kwa Majuma Mawili Zaidi