Mshambuliaji kutoka nchini Argentina, Ezequiel Lavezzi, atakuwa akilipwa mshahara wa pauni 400,000 kwa juma, baada ya kukubaliana na viongozi wa klabu yake mpya ya Hebei China Fortune inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini China mapema mwezi huu.

Lavezzi, ambaye amekua katika wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha mabingwa wa soka huko nchini Ufaransa, Paris St-Germain (PSG) chini ya meneja Laurent Blanc, amekubali dili hilo ambalo linamuwezesha kulipwa mara mbili na nusu ya mshahara ambao alikua akilipwa Parc des Princes.

Kwa mujibu wa gazeti la Times, imeelezwa kuwa wakala wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, amefikia makubaliano ya mchezaji wake kulipwa kitita hicho baada ya taratibu za awali za uhamisho kukamilishwa juma moja lililopita.

Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kwa Lavezzi kuondoka nchini Ufaransa na kuelekea nchini China, kutokana mipango iliyokua ikiendelea chini kwa chini dhidi ya viongozi wa klabu ya Chelsea ambao walionyesha nia ya kutaka kumsajili.

Lavezzi atakuwa nje ya mkataba wa kuitumikia klabu ya Paris St-Germain mwishoni mwa msimu huu na tayari klabu ya Hebei China Fortune iliyopanda kucheza Ligi Kuu ya China msimu uliopita, imeshalipa pauni milioni 3.5 kama ada yake ya uhamisho.

Klabu hiyo kupitia akaunti yake ya Weibo imetangaza kufanikisha dili hilo na kutamba kuwa kuwasili kwa Lavezzi kutaifanya kuwa na safu kali ya ushambuliaji.

TCAA yapata Mkurugenzi Mkuu Mpya
Abramovich Ajipanga Kuvunja Benki Kwa Ajili Ya Toni Kroos