Waziri mkuu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea magari 51 ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa shughuli za uhifadhi wa utalii, huku akieleza furaha yake kwa faru mmoja kupewa jina lake, huku faru mwingine akipewa jina la Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess.

Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania inashukuru kwa msaada wa fedha za nyongeza kiasi cha Euro milioni 15 zilizotolewa na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kukabiliana na athari za Uviko-19.

Msaada huo ni kwa ajili ya uboreshaji wa shughuli za uhifadhi wa utalii Tanzania katika hifadhi za Taifa Serengeti, Nyerere na Pori la Akiba Selous wenye thamani ya Euro 20 milioni sawa na Sh56 bilioni.

Awali akizungumza katika upokeaji wa msaada huo leo Desemba 20 Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana amebainisha kuwapa faru wawili majina ya viongozi hao.

Naye Waziri Mkuu Majaliwa baada ya kuelezwa hilo, amesema, “Hii ni heshima kwangu, naomba mmtunze ili nitakapokuja kumuona nimkute vizuri.”

Mradi huo unatekelezwa kwa pamoja kati ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) na shirika lisilo la Kiserikali la Frankfurt Zoological Society (FZS) kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW).

“Nimejulishwa na timu ya wataalamu kutoka TANAPA, TAWA na KFW kwamba mradi huu kwa sasa uko katika hatua ya maandalizi,” amesema.

Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess amesema Serikali ya nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu.

Ivan Toney anaswa tena sakata la KAMARI
Ntakarutimana Spika mpya Bunge la EALA