Mawaziri wa Fedha na magavana wa benki kuu wa kundi la mataifa yaliyoendelea na yale yanayoinukia G20 wanafanya mazungumzo leo Oktoba 14 ya kuchochea ufufuaji wa uchumi wa dunia uliodhoofika kutokana na janga la virusi vya corona.
Mazungumzo hayo kwa njia ya video yanafanyika siku moja tangu Shirika la fedha la Kimataifa IMF kuonya kuwa pato jumla la uchumi wa dunia litapungua kwa hadi asilimia 4.4 mwaka 2020 na athari za janga la corona zitaendelea kwa miaka kadhaa inayokuja.
Aidha, mwenyeji wa mkutano huo Saudi Arabia, imesema pamoja na mambo mengine maafisa hao watajadili mpango wa kusaidia uchumi wa ulimwengu na pendekezo la kurefusha muda wa kulipa madeni kwa mataifa masikini.
Mzozo wa kiafya uliochochewa na janga la COVID-19, umesababisha ukosefu mkubwa wa ajira duniani na juhudi za kupunguza makali ya athari za janga, bado hazijapata mafanikio makubwa.