Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, amewataka Wakuu wa Wilaya Mkoani humo kujibu hoja zote zilizowasilishwa kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 kabla ya kufika mwisho wa wiki ijayo.

Gambo ametoa agizo hilo wakati wa Kikao cha maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2017/2018 na mapitio ya bajeti ya mwaka wa Fedha 2016/2017 kilichohusisha Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha na wataalam kutoka Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

“Nataka kila Halmashauri ikamilishe kujibu hoja kwa wakati na kwa majibu sahihi sio kufanya majibu ambayo yanaibua hoja zaidi au hayajitoshelezi na kwa Halmashauri ambayo ilipata Hati Chafu au Hati ya Mashaka kwa mwaka uliopita ianishe wataalamu waliopelekea Halmashauri kupata Hati hizo ili waweze kuchukuliwa hatua Stahiki”amesema Gambo.

Aidha, amewataka wakuu wa Wilaya kushiriki kikamilifu kuhakikisha hoja zinajibiwa ipasavyo na waliosababisha na  upotevu wa fedha za umma wachukuliwe hatua mara moja ili kuleta nidhamu na kuongeza umakini katika zoezi la ujibuji hoja.

Hata hivyo, Gambo amezitaka Halmashauri ambazo hazijatoa asilimia kumi ya mapato yao kama mikopo kwa vikundi vya wananawake na vijana zikatoe Fedha hizo kabla ya mwisho wa Januari ili kuweza kuinua uchumi wa makundi haya yaliyoainishwa kwa mujibu wa Sera na Maelekezo.

 

Majaliwa kutuma kamati ya uchunguzi Kampuni ya TANCOAL
Waziri Mkuu azindua mradi wa maji kata ya Mkongotema