Mtendaji mkuu wa klabu bingwa nchini Italia, Juventus FC, Giuseppe Marotta amesema bado hawajapokea ofa yoyote inayomlenga kiungo wao kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba.

Marotta, amezungumza jambo hilo kwa kuweka taarifa za usajili wa mchezaji huyo sawa, kutokana na baadhi ya vyombo vya habari kuendelea kuvumisha harakati za uhamisho wake kwa kuzihusisha klabu za Chelsea, Man Utd pamoja na Real Madrid.

Marotta amesema taarifa zinazoendelea kuchapishwa kuhusu Pogba, hazina ukweli wowote na wanaamini zimekua zikipikwa kwa makusudi kwa maslahi ya kundi la watu fulani.

Hata hivyo amedai kwamba, hawana mpango wa kumuachia Pogba katika kipindi hiki, na wanaamini jambo hilo litafanikiwa kutokana na mchezaji huyo kuonyesha dhahir anahitaji kubaki mjini Turin.

“Hatujapokea ofa yoyote,” Alisema.

“Pogba ni mchezaji anaejitambua na sidhani kama linalozungumzwa linaweza kujitokeza, kwa sababu tunaamini bado anahitaji kubaki nasi, kama mkataba wake unavyoeleza.” Aliongeza Marrota

Taarifa za kuuzwa kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23, ziliibuliwa tena mwishoni mwa juma lililopita, ambapo baadhi ya vyombo vya habari vya nchini Ufaransa, England pamoja na Hispania viliripoti kwamba, huenda Pogba akaondoka Juventus Stadium, wakati wa majira ya kiangazi kwa ada itakayovunja rekodi.

Pauni milioni 125, zilitajwa huenda zikatumika katika uhamisho wake, lakini haikuelezwa ni klabu gani imejipanga kutoa kiasi hicho cha pesa.

Adolf Rishard Atangaza Mipango Ya Msimu Wa 2016-17
Kitwanga afunguka kwa mara ya kwanza, ‘tumefundishwa kusamehe’