Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amekiri atamkosa kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pape Osman Sakho kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy FC ya Botswana.
Simba SC wataanzia ugenini mjini Gaberone Oktoba 15, kisha watamalizia nyumbani jijini Dar es salaam Oktoba 22, mwaka huu, kwa kucheza mchezo wa mkondo wa pili Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha Gomes amesema anasikitika atamkosa kiungo huyo machachari kwenye mchezo huo, kufuatia majeraha aliyoyapata kwenye mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC.
Amesema jeraha la Sakho bado linampa wakati mgumu wa kurejea uwanjani siku za karibuni, hivyo hatomtumia kwenye mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Simba SC.
“Tupo tayari kwa mechi kubwa na muhimu kwetu nimewaandaa wachezaji wangu vizuri, ili kuhakikisha tunaanza vyema ugenini.”
“Pape Ousmane Sakho anajeraha kubwa alilopata kwenye mchezo wetu na Dodoma Jiji hivyo itamchukua muda kurejea, ila kwa wachezaji wengine ni matatizo ya kawaida.” amesema Kocha huyo aliyeifikisha Robo fainali Simba msimu uliopita.
Sakho alilazimika kutolewa kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC, baada ya kuchezewa rafu mbaya kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere.