Meneja wa klabu ya Man City Pep Guardiola amesema bado hajaridhishwa na kiwango cha kikosi chake, na anashangazwa na baadhi ya wadau wa soka duniani kuanza kuamini huenda msimu huu akafanikisha azma ya kutwaa ubingwa wa ligi ya nchini England pamoja na ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Guardiola ambaye mwishoni mwa juma lililopita alikiongoza kikosi chake kuibomoza Man Utd katika uwanja wa Old Trafford kwa kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja, amesema ni mapema mno kwa Man City kupewa matarajio hayo.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania ameonyesha kutoridhishwa na matarajio ya wadau wengi wa soka kuhusu kikosi chake, alipokua katika mkutano na waandishi wa habari ambao ulilenga kuzungumzia mpambano wa mzunguuko wa kwanza wa hatua ya makundi wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, ambao utawakutanisha na Borussia Monchengladbach leo usiku.

“Sikubaliani na matarajio na wadau wengi wa soka kuhusu kikosi changu kuwa miongoni mwa wanaofikiriwa kuwa mabingwa kwa msimu huu, bado hatujawa sawa sawa kama ninavyotaka,”

“Ni vigumu kwa msimu wa kwanza kufanya maajabu kama ya kutwaa ubingwa katika ligi ngumu kama ya England, pia katika ligi ya mabingwa barani Ulaya kuna changamoto kubwa ya kuwepo kwa klabu zenye vikosi vyema uwezo mkubwa na vimekaa kwa muda mrefu tofauti na Man City ambayo kwa sasa inajitengeneza.” Alisema Guardiola

Hata hivyo Guardiola amekiri kufurahishwa na matokeo ya kikosi chake tangu msimu huu ulipoanza kazi, ambapo katika ligi ya nchini England wamebahatika kupata point 12 zilizotokana na ushindi mfululizo katika michezo minne, huku akishinda michezo miwili ya hatua ya mtoano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Steaua București jumla ya mabao sita kwa moja.

“Kwa kawaida sina budi kufurahia matokeo yaliyopatikana mpaka hivi sasa, natambua tumeanza vizuri ligi ya England na kushinda michezo miwili ya mtoano ya ligi ya mabingwa Ulaya, lakini hicho sio kipimo kizuri cha kuanza kuamini Man City imekamilika na kufikia hatua ya kufikiriwa kuwa mabingwa.”

Guardiola amekua na historia nzuri ya ukufunzi, tangu alipoanza shughuli hiyo akiwa na FC Barcelona mwaka 2008-2012 kabla ya kutimkia FC Bayern Munich mwaka 2013-2016 na sasa yupo Man City.

Kwa ujumla Guardiola ameshafanikiwa kutwaa mataji 21 na miongoni mwa hayo mataji ya Ulaya yapo mawili.

Kaseja Aitwa Timu Ya Taifa Soka La Ufukweni
Arsene Wenger: Nilikataa Kazi PSG Kwa Sababu Ya Arsenal