Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amekanusha ripoti za hivi karibuni katika mitandao zikidai kwamba wanajeshi na raia kadhaa wa Tanzania waliuawa nchini Msumbiji na waasi huko Cabo Delgado.

“Hivi ninavyozungumza sasa, hakuna afisa wa jeshi au raia yeyote kutoka Tanzania ambaye ameuawa kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji,” amesema Byakanwa.

Akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari, Byakanwa amesema kuwa serikali imeimarisha usalama kupitia operesheni kadhaa kuu za usalama katika maeneo yote.

Byakanwa amesema kuwa mpaka wa Tanzania na Msumbiji uko salama hata kama mashambulizi yanaendelea katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado.

“Vyombo vyetu vya usalama viko macho na vimejipanga vizuri kuhakikisha mpaka wa Tanzania na nchi jirani uko salama,” amesisitiza Byakanwa.

Byakanwa ameeleza kuwa maafisa wa usalama mpakani walikuwa wakifuatilia kwa umakini wasafiri wote wanaoingia nchini kutoka Msumbiji, akiwataka watanzania wanaoishi mpakani kukaa macho na kuripoti shughuli zozote za kutiliwa shaka katika maeneo yao kwa sababu za usalama.

“Natoa wito kwa wananchi, haswa wale walioko karibu na Mto Ruvuma kutupa habari kuhusu watu wanaoingia nchini kinyume cha sheria na watu ambao wanahatarisha usalama wa umma, “amesema Byakanwa.

Byakanwa ameshauri watanzania wanaosafiri kwenda Msumbiji, kutumia Kilambo na madaraja ya Mtambaswala, na kwamba watu katika jamii za mpakani wanapaswa kuzingatia maagizo yote yanayotolewa na serikali za mitaa na serikali kuu.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 11, 2020
Baba amuua bintiye kwa kuchelewa kurudi nyumbani