Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar kusambaza tarifa za matokeo ya Sensa na kuhamasisha taasisi za Serikali na Binafsi juu ya matumizi sahihi ya takwimu hizo katika kuendeleza shughuli za kibishara na uchumi.
Othman ametoa maelekezo hayo hayo Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, wakati akikabidhiwa nakala za vitabu kumi na moja vya taarifa tofauti za matokeo ya Sensa ya mwaka 2022, kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Saada Mkuya Salim aliyembatana na Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohammed Hamza na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Salim Kassim Ali.
Amesema, iwapo taarifa hizo za matokeo ya sense zitatumika ipasavyo zitaweza kuleta manufaa makubwa katika nchi hasa katika upangaji wa mipango ya maendeleo katika shughuli za kibiashara na toaji wa huduma mbali mbali za kijamii katika ngazi tofauti.
Aidha, ameongeza kuwa jamiii na taasisi za Serikali na binafsi kwa jumla zinahitaji kuhamasishwa na kuwa na mwamko juu ya kuwepo haja na umuhimu mkubwa wa kutumia taaisfa hizo katika masuala mbali mbali na kuwa chachu ya mabadiliko ya kimaendeleo nchini.