Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amewataka mashabiki wa timu hiyo kujiandaa kuishangilia tena timu yao katika michuano ya Afrika mwaka 2017.

Poppe, amedai kuwa pamoja na mazingira magumu wanayokabiliana nayo hivi sasa, watahakikisha wanapata tiketi ya kurudi kwenye michuano ya Afrika mwaka 2017.

Amedai kuwa hadi sasa kwenye Ligi Kuu mwenendo wa timu yao siyo mbaya, kwani wana nafasi ya kuchukua ubingwa iwapo watajipanga vizuri kwa ajili ya michuano ya Kombe la TFF, ili wachukue ubingwa.

Poppe, amedai kuwa baada ya miaka mitatu ya kuwa nje ya michuano ya Afrika, sasa wamepania kurudi na kukata midomo ya watu wanaodhani kuwa hawawezi kurudi kileleni.

Amedai kuwa historia inavyoonyesha kuwa, Simba SC ikipotea kwa muda mrefu kwenye michuano ya Afrika, inarudi kwa nguvu na kuweka rekodi, na kusema kuwa wanawaomba wana Simba wawe na subira, 2017 siyo mbali.

Amesisitiza kuwa uongozi wa Simba SC umeunganisha nguvu ya wachezaji na makocha wao ili kuhakikisha kwa pamoja wanapambana hadi dakika ya mwisho wavune kitu.

Ameongeza kuwa hawataki kujivuruga wala kuvurugwa safari hii, wamejifunza kutokana na makosa na sasa wametulia ili mwisho wa msimu wavune kitu kwani wana kiu ya kurudi kwenye michuano ya Afrika.

Julio Ampongeza Rais Magufuli Kuhusu Nape
Samuel Eto’o Abebeshwa Zigo La Ukocha