Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba jukumu la Kamati yake si kupendekeza mchezaji wa kusajiliwa, bali kuhakikisha zinapatikana fedha za kusajili.

Hans Poppe amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya shutuma zinazoendelea kwenye baadhi ya vyombo vya Habari nchini, kwamba amekuwa akisajili kwa utashi wake.

Poppe amesema kwamba jukumu la kutafuta na kupendekeza wachezaji wa kusajiliwa ni la Kamati ya Ufundi, ambayo ipo chini ya Mwenyekiti, Collin Frisch, Makamu Mwenyekiti, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Wajumbe Mohamed Yakoub, Patrick Rweyemamu, Osman Kazi, George Lucas na Duwa Said.

Poppe amesema kwamba baada ya Kamati hiyo kutafuta na kupata wachezaji wa kusajiliwa, huwasilisha orodha kwenye Kamati ya Utendaji ya klabu chini ya Rais, Evans Aveva ambayo ndiyo hupitisha orodha rasmi ya wachezaji wa kusajiliwa.

“Baada ya sasa Kamati ya Utendaji kupitisha wachezaji wa kusajiliwa, ndiyo tunaletewa sisi Kamati ya Usajili kuhakikisha tunawafikia hao wachezaji waliopendekezwa popote, tuwasajili. Hapo sasa ndipo utasikia au kuona Hans Poppe amesafiri kwenda hata Brazil, au Zimbabwe kufuata mchezaji,”amesema.

“Mimi nilikwenda Brazil kufuata mchezaji mwaka juzi, ambaye kwa bahati mbaya hatukumpata. Na nilikwenda baada ya Kamati ya Ufundi kumpendekeza mchezaji waliyeletewa video zake na wakala,”amesema.

“Na wiki iliyopita nilikwenda Zimbabwe na baadhi wa Wajumbe wa Kamati ya Ufundi, kwenda kujaribu kufanya mazungumzo na wachezaji waliopendekezwa na kupitishwa na Kamati ya Utendaji,”

“Na kwa sasa, kimya kimya ninaendelea na mazungumzo na wachezaji ambao wamependekezwa na Kamati ya Ufundi kupitishwa na Kamati ya Utendaji wasajiliwe. Na nitasafiri pia kwa ajili ya zoezi hilo hilo, lakini ninawafuata wachezaji waliopendekezwa na kupitishwa katika utaratibu tuliojiwekea,”ameongeza Hans Poppe.

Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amewashauri Waandishi wa Habari waonyeshe weledi kwa kuandika habari kwa ufasaha na si kufanya kwa utashi wao, bila kuzingatia wanapotosha.

“Inashangaza mtu anaporudia kusema eti mimi ninasajili kwa utashi wangu, hii si sawa hata kidogo, Simba ina utaratibu mzuri tu iliyojiwekea katika kusajili na si Hans Poppe wala Kaburu (Geoffrey Nyange), au Said Tuliy anayesajili,”amesema.

“Kuhusu kusajili wachezaji ambao wanashindwa kucheza vizuri, hayo mambo yanatokea hata Ulaya, unaweza kuniambia Angel Di Maria alikuwa mchezaji mbaya wakati anasajiliwa Manchester United kutoka Real Madrid? Hapana.”

“Alikuwa mchezaji mzuri tu, lakini akashindwa tu kufanya vizuri Manchester United. Tazama huyu kijana Mholanzi, Memphis Depay alisajiliwa kwa matumaini makubwa Manchester United, lakini sasa anapakia gari zake kurudisha Uholanzi baada ya kushindwa kufanya vizuri katika msimu wake wa kwanza Old Trafford,”amesema.

Poppe ameongeza kwamba Simba SC ipo katika kipindi kigumu cha mpito kwa sasa na kwa sababu hiyo mengi yatakuwa yanazungumzwa na vyombo vya Habari, lakini ameshauri kusiwe na upotoshaji.

“Sisi kama Simba hatukatai kukosolewa tunapokosea, lakini iwe kwa ufasaha bila kumpaka mtu matope au kuzungumza kishabiki, hiyo si sawa,”amesema Poppe.

Pamoja na hayo, Poppe amesema kwamba wanaendelea na zoezi la usajili kulingana na mapendekezo ya Kamati ya Ufundi, yaliyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya Simba na muda utakapofika mambo yatawekwa hadharani.

AC Milan Wamvuta Manuel Pellegrini Kimya Kimya
Video: ‘zigo remix’ ya Ay na Diamond imefanywa upya Kenya, Hii hapa Video yake