Kocha wa mabingwa wa soka Tanzania bara, Young Africans, Hans van Pluijm amefichua siri ya kikosi chake kukubali kupoteza mchezo wa pili wa michuano ya kombe la shirikisho la soka barani Afrika CAF, kwa kufungwa na TP Mazembe jijini Dar es salaam.

Pluijm amefichua siri hiyo alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo wa jana ambao ulihudhuriwa na mashabiki lukuki kutoka sehemu mbalimbali za jiji hilo, kufuatia kiingilio cha uwanjani kufanywa bure.

Babu huyo kutoka nchini Uholanzi, alisema kosa kubwa lililofanywa na wachezaji wake, ni kushindwa kutumia nafasi walizozipata walipofika langoni mwa TP Mazembe ambao walitoa upinzani mkubwa wakati wote.

Alisema, timu yake ilizidiwa kwenye eneo la kiungo kutokana na viungo wake kupoteza ubora wakati wa kipindi cha pili.

“Timu yangu ilipambana sana lakini kwa bahati mbaya tukaruhusu goli kipindi cha pili, tulishindwa kutumia nafasi kama mbili au tatu tulizopata kipindi cha kwanza”, “Ukicheza na timu kama TP Mazembe halafu hupati nafasi nyingi, ukipata nafasi unatakiwa kuitumia kufunga, kama haufungi magoli hauwezi kushinda mchezo,

“Kwa upande mwingine, TP Mazembe wana timu yenye wachezaji wenye nguvu. Tulipoteza ubora wetu kwenye eneo la kiungo.”

“Tulifanya mabadiliko lakini haikusaidia, ni sehemu ya mchezo nampongeza sana kocha wa Mazembe.” alisema Hans kwenye mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mchezo wa Yanga vs TP Mazembe kumalizika.

Kupoteza mchezo wa jana, kunaifanya Young Africans kuburuza mkia wa kundi A, baada ya kushika dimbani mara mbili na kutoambulia point yoyote.

Kundi A la michuano ya kombe la shirikisho lina timu za Mo Bejaia (Algeria), TP Mazembe (DR Congo), Medeama (Ghana) pamoja na Young Africans (Tanzania).

Fastjet yatangaza punguzo kubwa la nauli mwezi Septemba kwa ‘maelfu ya siti’, Wahi dili
Mahakama Yapinga Uhamisho wa ''El Chapo''