Kiungo wa Mbeya City, Hassan Maulid Machezo ‘Rasta’ amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kutokana na kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans uliopigwa juzi Jumanne (Juni 06).
Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na ulimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3.
Katika mchezo huo, Machezo alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 80 na mwamuzi Tatu Malogo kutokea Tanga kutokana na kuzichapa na winga wa Yanga Jesus Moloko, ambaye naye alitolewa kwa kadi.
Wakati akitolewa, Mbeya City ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-1 na alikuwa akisaidiana vizuri na Abdurazack Hamza na Richarson Ng’odya kuwazima viungo wa Young Africans walioongozwa na Khalid Aucho.
Hassan Maulid
Kiungo huyo amesema anawaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kwa kupewa kadi nyekundu, kwani dhamira yake ilikuwa ni kuipambania timu yake.
“Naomba radhi, inawezekana kutokana na dhamira yangu ya kuipambania timu ndiyo ilisababisha kile, lakini narudia kuomba radhi kwa wachezaji wenzangu, benchi la ufundi pamoja na mashabiki,” amesema kiungo huyo wa zamani wa Dodoma Jiji.
Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kuwa katika mstari wa hatari wa kucheza ‘play-off’ kutokana na kufikisha alama 31 katika nafasi ya 13, huku KMC ikiwa ya 14 kwa alama 29 na Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zikiwa tayari zimeshuka daraja.
Mchezo wa mwisho wa kumaliza msimu, Mbeya City itacheza na KMC, mwechi inayotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, ikiwa ni ya kuamua.