Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera (Robertinho), anatarajia kukumbana na wakati mgumu wa kumzuia kiungo Jonas Mkude asiondoke katika timu hiyo baada ya kuwapo kwa taarifa za nyota huyo kutakiwa na Singida Big Stars.

Mkataba wa Mkude na Simba SC unamalizika mwishoni mwa msimu huu na tayari Robertinho amesema kiungo huyo yupo katika mipango yake ya msimu ujao.

Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Mkude ameanza mazungumzo na Singida Big Stars lakini waajiri wake wa sasa wakiwa wameonyesha nia ya kumhitaji abakie kikosini.

“Mkude amekuwa chaguo la kwanza kusalia ndani ya kikosi cha Simba, baada ya kocha (Robertinho) kuwataka viongozi kuhakikisha anabaki licha ya kutokuwa na nafasi kwenye kikosi cha kwanza, kocha ametaka kiungo huyo kutoenda kokote kwa sababu anaimani wachezaji wazawa wanaweza kusaidia timu,” kimesema chanzo hicho.

Kiliongeza kuwa bado Mkude hajafanya uamuzi wa timu ipi asaini mkataba kwa sababu anataka kujiridhisha anamwaga wino katika timu itakayompa maslahi mazuri.

“Mkude amesema atazingatia maslahi, mpira ni kazi yake, ofa nzuri kati ya timu hizo mbili ndio itaamua hatima yake,” kimeongeza chanzo chetu.

Tayari Singida Big Stars yenye makao yake mkoani Singida imeshafanikiwa kuinasa saini ya Mlinda Lango namba mbili wa Wekundu wa Msimbazi, Beno Kakolanya.

Singida Big Stars inajipanga kuimarisha kikosi chake ili ifanye vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika watakayoshiriki msimu ujao.

Serikali haijasaini mkataba wa miaka 100 - Mkurugenzi TPA
Wajumbe CWT wamekiuka kanuni - Mwenyekiti Mstaafu