Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amewataka wananchi kulisaidia jeshi hilo kumkamata mtu aliyemtishia bastola mbunge wa Mtama, Nape Nnauye.

Akizungumza leo mkoani Mtwara, IGP Sirro amesema kuwa mtu huyo anayeonekana kwenye picha akimtishia Nape kwa bastola amekimbia na hajulikani alipo, hivyo yeyote atakayemuona alitaarifu jeshi hilo.

“Wananchi watusaidie, hata nyie wananchi wa Mtwara mkimuona mtu huyo mliyemuona kwenye picha toeni taarifa mtusaidie kumpata,” alisema IGP Sirro.

“Picha kuonekana haimaanishi kuwa mtu yule ataonekana kirahisi, lakini upelelezi unaendelea kumtafuta mtu huyo aliyemtishia mheshimiwa Nape. Wananchi watusaidie, maana suala la kumpata mhalifu ni ushirikiano, sisi tunaenda kwa taarifa. Bila taarifa hatuwezi kufanikiwa,” aliongeza.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alisema kuwa mtu huyo aliyemtishia Nape kwa bastola hadharani sio askari wa jeshi la polisi.

Nape alitishiwa kwa bastola na mtu huyo Machi 23 mwaka huu jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wake kama Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo, Vijana na Utamaduni.

Mkutano wake na waandishi wa habari uliokuwa umepangwa kufanyika katika eneo hilo ulizuiwa na Jeshi la Polisi.

Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 5, 2017
IGP Sirro amtumia ujumbe dereva wa Lissu, ‘inanipa tabu’