Mshambuliaji Japhar Kibaya hatokuwa sehemu ya kikosi cha Ihefu FC kitakachoikabili Simba SC Jumamosi (Novemba 12), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kibaya aliyesajiliwa Ihefu FC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar, amekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Klabu hiyo ya mkoani Mbeya, ambacho kinaendelea kupambana ili kujinasua kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Kocha Mkuu wa Ihefu FC Juma Mwambusi amesema Mshambuliaji huyo amelazimika kuondoka Kambini, kutokana na kupatwa na msiba wa mtoto wake, hivyo hatoweza kuwahi mchezo dhidi ya Simba SC.

Amesema ni kama bahati mbaya kwa kikosi chake kumkosa Kibaya, lakini ameahidi kupambana dhidi ya Wababe hao wa Msimbazi ili kupata alama tatu ugenini.

“Ni bahati mbaya kwetu kumkosa Kibaya kwa sababu wakati tuko kambini alipata taarifa za kuondokewa na mtoto wake, hivyo tutapambana kadri ya uwezo wetu na wengine ambao wako kikosini,”

“Tunatarajia mchezo mgumu na wenye ushindani lakini kwa nafasi ambayo tupo tunapaswa kujiandaa vyema kuanzia kwenye aina ya uzuiaji wetu na wakati huo huo tukipambana kutafuta mabao yatakayotuweka sehemu nzuri.” amesema Kocha Mwambusi

Ihefu Inaburuza mkia wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama tano, baada ya kushuka dimbani mara tisa tangu msimu huu 2022/23 ulipoanza mwezi Agosti.

Simba SC itakayokua mwenyeji wa mchezo wa Jumamosi (Novemba 12) inashika nafasi tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 18, ikicheza michezo nane hadi sasa.

Ahmed Ally: Banda atasubiri mwezi mzima
Air Tanzania yapunguza Safari za ndege