Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohamed Javad Zarif, ameionya Marekani kuwa haitokuwa salama baada ya kuanzisha vita ya kiuchumi dhidi ya Iran.
Ametoa kauli hiyo dhidi ya Marekani wakati wa ziara ya waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas, jijini Tehran anayejaribu kupunguza mvutano unaoongezeka katika eneo la Ghuba.
Amesema kuwa njia pekee ya kutuliza hali ya wasiwasi iliyopo ni kwa kuondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran na kuongeza yule aliyeanzisha vita hivyo dhidi Iran hatoweza kuvimaliza.
Aidha, chanzo cha mvutano uliopo ni uamuzi wa Marekani wa kujitoa kutoka mkataba wa nyuklia na Iran na kuongeza vikwazo vya kuchumi dhidi ya taifa hilo la Ghuba ya Uajemi.
Kwa upande wake, Maas amesisitiza kuwa Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya yanataka kutafuta njia ya kuyanusuru makubaliano ya nyuklia ambayo yameshuhudia Iran ikipunguza urutubishaji madini ya Urani ili iondolewe vikwazo vya kiuchumi.