Idadi ya vifo vya shambulizi la bomu katika kanisa la Protestanti nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), la siku ya Jumapili imeongezeka na kufikia watu 14 huku kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS likidai kuhusika na shambulio hilo.
Katika tukio hilo, watu wasiopungua 63 walijeruhiwa na lililotokea katika mji wa Kasindi uliopo mashariki mwa nchi hiyo ya DRC na IS kupitia mtandao wake wa kueneza propaganda imesema wanamgambo wake walitega bomu ndani ya kanisa na kulipua wakati wa ibada.
Aidha, pia wamedai kuwa idadi ya vifo ni ya juu zaidi ya iliyoripotiwa na Serikali ambapo mji huo wa Kasindi upo katika mkoa ambao vikosi vya DRC na vya Uganda, vimekuwa vikipambana na makundi kadhaa ya wanamgambo likiwemo la Allied Democratic Forces (ADF) lenye mafungamano na IS.
Hata hivyo, ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na Umoja wa Mataifa UN ilisema kundi la ADF limewaua raia wasiopungua 370 tangu Aprili mwaka 2022 na pia liliwateka nyara mamia ya watu.