Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva ametoa onyo kwa wagombea walioshindwa katika uchaguzi mkuu uliopita kuacha kuwapotosha wananchi kwa madai kuwa walioshinda.

Akiongea kwenye mkutano wa tathmini kati ya NEC na asasi za kiraia kuhusu utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa wananchi uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma, Jaji Lubuva alisema kuwa viongozi hao wanawapotosha wananchi na kwamba hata wananchi wenyewe waliofanya maamuzi kupitia sanduku la kura wanawashangaa.

“Wananchi ndio walioamua, sisi tulichokifanya ni kusoma maamuzi ya wananchi. Sasa wagombea walioshindwa wanapoanza kuwapotosha wananchi kuwa walishinda wananchi wanawashangaa,” alisema. “Wananchi wanawashangaa kwa sababu wao ndio walioamua ni nani anafaa kuwaongoza,” aliongeza.

Kauli hiyo ya Jaji Lubuva imekuja siku chache baada ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kuwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa yeye ndiye aliyeshinda katika uchaguzi uliopita lakini matokeo yalichakachuliwa.

Akijibu kauli iyolitolewa na Lowassa ingawa hakumtaja jina, kuwa watendaji wa NEC wafukuzwe kazi kwa kushindwa kusimamia vizuri uchaguzi na kushirikiana na upande mmoja kuchakachua matokeo, Jaji Lubuva alioenesha kuishangaa kauli hiyo na kuwata walioshindwa kufahamu kuwa katika kila uchaguzi kuna kushinda na kushindwa.

“Sashangaa kuna baadhi ya wagombea wanataka Tume ifukuzwe kazi eti tu kwa sababu wao hawakushinda. Naomba ifahamike kwamba katika kila uchaguzi duniani kuna kushinda na kushindwa. Sasa kama kila anayeshindwa atataka Tume ifukuzwe kazi hakutakuwa na Tume ya uchaguzi,” Lubuva alieleza.

 

Angalia video mpya ya Wimbo wa Ali Kiba 'Lupela'
Video: Beyonce alivyonusurika ajali Jukwaani kwenye Super Bowl