Beki wa kati wa Wagonga Nyundo Wa Jijini London (West Ham United) James Collins, ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa lake la Wales, na kuamua kujikita kwenye ligi ya England kwa kuisaidia klabu yake ambayo inapambana ili kufikia lengo linalokusudiwa msimu huu wa 2017/18.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Wales Chris Coleman, amethibitisha kupokea taarifa za kustaafu kwa Collins, baada ya kubainishiwa na viongozi wa chama cha soka nchini humo.
Collins ametangaza kustaafu huku akiacha kumbukumbu ya kucheza michezo 50 akiwa amevaa jezi ya timu ya taifa ya Wales, na alimaliza vyema kwa kuchangia ushindi katika mchezo wao kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2018 dhidi ya Moldova mwezi Septemba.
“Inasikitisha sana kupokea taarifa kama hizi, kwa hakika nilikua nimeshamzoea kutokana na uwajibikaji wake anapokua uwanjani, lakini sina budi kuheshimu maamuzi aliyoyachukua katika kipindi hiki,”
“Alitumia muda mwingi kuwashauri wenzake alipokua uwanjani, nilifurahishwa na jambo hilo kama kocha, lakini nitaendelea kumtumia hata katika ushauri ili tufanikishe mpango wa kuiendeleza timu yetu.”
“Naamini watakaofuata baada yake watakua wamejifunza mambo mengi kutoka kwa Collins na wataiwezesha Wales kufanya vyema katika michezo itakayotukabili siku za usoni, ambapo tutacheza bila yeye.” Amesema Coleman.
Collins mwenye umri wa miaka 34, kwa msimu huu amecheza michezo mitatu akiwa na kikosi cha West Ham Utd, na mara ya mwisho alionekana katika mchezo dhidi ya Liverpool, ambao ulishuhudia wakipoteza point tatu.