Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt.  Fadhil Abdallah ameitaka jamii kubadili tabia kwa  kuweka mazingira yanayowazunguka safi na kuhakikisha wanatumia maji safi na salama ili kujiepusha na maradhi ya mripuko .

Ameyasema hayo wakati  wa kikao cha kamati ya kitaifa ya kuandaa mpango mkakati wa kudhibiti maradhi ya kipindupindu  hasa kipindi  hiki ambacho mvua za masika zimeanza kunyesha.

Amesema kuwa lengo kuu la kamati hiyo ni kufanya tathmini ya muendelezo wa mpango kazi wa kudhibiti maambukizi ikiwemo kutoa elimu ya usafi wa mazingira kwa jamii na  kupambana na mazingira hatarishi katika maeneo mbali mbali ya Manispaa za Zanzibar.

“Wananchi wahakikishe wanakunywa maji ya kuchemsha au kuyatia watergard ili kuweka tahadhari wakati huu wa kipindi cha mvua za masika kwani kuna uwezekano mkubwa wa kuchafuka vyanzo vya maji kwa kuingia maji machafu,”  Amesema Dkt. Abdallah .

Aidha, ameishauri Mamlaka ya Maji Zanzibar  (ZAWA) kuhakikisha maji yanayotumiwa na wananchi yapo katika hali ya safi na salama kwa  kutia dawa vyanzo vyote vya maji  na kuwataka wananchi kuacha tabia  ya kufanya uharibifu kwenye njia za maji kwa kutoboa  mabomba yanayosambaza maji .

Hata hivyo, ametoa rai kwa wananchi wanaoishi sehemu za mabondeni kuchukua juhudi za makusudi kuhama katika maeneo hayo ili kuepuka majanga  katika kipindi hiki cha mvua za masika.

Lissu akabidhiwa zigo na Kaimu Jaji Mkuu
Emre Aanika ndoto yake kwa Real Madrid na Barcelona