Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Lebaratus Sabas ametaja idadi ya watu waliofariki katika ajali ya gari iliyoanguka nakupelekea kulipuka kwa moto leo Agosti 10, ambapo amesema imefikia 62.
Amesema kuwa kati ya hao waliofariki wanaume ni 58 na wanne ni wanawake ambapo mmoja katika wanawake hao ni mtoto.
Kwa upande wa idadi ya majeruhi amesema kuwa imefikia 72, wanawake wakiwa 8 na wanaume 64 ambapo wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hosptali ya rufaa ya Morogoro.
Aidha, ajali hiyo imetokea majira ya asubuhi katika eneo la Msamvu Mkoani Morogoro na hadi sasa Jeshi la polisi, limekwishakamata lita takribani 206 za mafuta ya petroli, zilizokuwa zimefichwa katika mabanda yaliyopo pembezoni mwa eneo la ajali ilipotokea.
”Pia katika eneo la tukio zimepatikana pikipiki zilizoungua kwa moto zipatazo 26 na baiskeli 6, pia yamaeonekana mabaki ya madumu na ndoo za plastiki zilizoungua,” amesema Kamishna Sabas.
Hata hivyo, Kamishina Sabas amewataka wananchi wanaoishi kandokando ya barabara kutokuwa na tamaa na kujiepusha na ajali ambazo zinaepukika, pamoja na kuwataka wale wote waliopata majeraha madogo madogo na kutokomea wasisite kwenda hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.