Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameungana na Watanzania wote kutoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza ndugu zao, katika ajali ya moto iliyotokea eneo la Msamvu Mkoa wa Morogoro, baada ya Lori kuanguka na kulipuka moto.

Rais Magufuli ametuma salamu hizo za rambirambi leo Agosti 10, 2019, na kuzitaka Wizara zote zinazohusika, kushughulikia ajali hiyo pamoja na kuzitaka Hopitali ya Mkoa wa Morogoro na Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu na kuokoa maisha yao.

”Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za marehemu wote, nawaombea marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka,” amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na vitendo vya watu kuvamia magari yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa.

”Baadhi ya magari haya yanabeba mafuta ambayo ni hatari, ilivyotokea Morogoro, yapo magari yanabeba kemikali za sumu, yapo magari yanabeba mlipuko, nawaomba sana tuache tabia hii” amesisitiza Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, hadi sasa ni zaidi ya watu 60 wamefariki na wengine 70 kujeruhiwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aitaka HESLB ijitafakari
Msemaji wa Serikali atoa neno kufuatia ajali ya lori la mafuta