Viongozi wa kijeshi wa Niger wamesema wamezima jaribio la rais aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum la kujaribu kutaka kutoroka kutoka kizuizini, hapo jana Oktoba 19, 2023.

Kwa mujibu wa Msemaji wa utawala wa Kijeshi wa Niger, Amadou Abdramane amesema Bazoum, aliyepinduliwa Julai 26, 2023 alijaribu kutoroka usiku pamoja na familia yake, wapishi na walinzi.

Amesema jaribio hilo lilishindikana na washiriki wakuu na baadhi ya washirika kukamatwa na wameshitakiwa, ambapo uchunguzi kuhusu tukio hilo umeanzishwa.

Awali ilidaiwa kuwa Bazoum alijificha nje ya mji mkuu Niamey na alikuwa amepanga kuondoka kwa kutumia ndege za helikopta zinazomilikiwa na Taifa jingine.

Septemba mwaka huu, mawakili wake walitangaza kufungua kesi mahakamani dhidi ya wale waliomwondoa madarakani na pia walipeleka kesi yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Jaribio hili la kutoroka linatokea wakati kikundi cha kwanza cha wanajeshi wa Ufaransa kilipowasili nchini Chad jirani siku ya Alhamisi, baada ya kuagizwa kuondoka na viongozi wa kijeshi wa Niger.

Ufaransa imeendelea kutoa msaada kwa kiongozi aliyeondolewa madarakani tangu mapinduzi na inaendelea kuomba kuachiliwa kwake.

Tanzania yakusudia kujiunga na mkataba Nishati Jadidifu
Mwinyi Zahera awasilisha barua ya utetezi