Serikali ya Tanzania imesema licha ya kushiriki kwenye jukumu mama la ulinzi wa mipaka ya Tanzania na kueneza amani ndani na nje, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limekuwa likitumika pia katika kulinda Uhuru na Katiba ya nchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax wakati akizungumzia ufanisi wa JWTZ kwenye mahojiano maalumu na kituo cha Dar24 Media na kuongeza kuwa Amani iletwayo na JWTZ inasaidia wawekezaji kuongezeka, uchumi kupanda, na wananchi kujishuhgulisha na shughuli za kimaendeleo bila ya bughudha.
“Nchi yetu inaongozwa na katiba, kwahiyo kulinda katiba inamaana kwamba unaisimamia ile misingi iliyowekwa kikatiba, kama kutakuwa na jaribio la kwenda kinyume na katiba, jeshi lina wajibu wa kuhakikisha kuwa katiba ya nchi yetu inalindwa,” amesema Waziri Dkt Stergomena.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa mchango wa jeshi kwenye uchumi wa Tanzania ni mkubwa licha ya kutokuwepo kwa takwimu halisi za kiwango cha uchangiaji wake, lakini kushiriki kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo na ujenzi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa kunatoa tafsiri ya makadirio ya mchango unaofikia karibu asilimia 70 kwenye uchumi wa nchi
“Huwezi kutenganisha ulinzi na maendeleo, hivi vyote vinaenda pamoja. Kama mazingira ya nchi yako hayana amani ni vigumu sana kuendelea, Wawekezaji wanapoenda kwenye nchi yoyote kitu cha kwanza wanaulizia nchi kama ina amani ya kutosha,hakuna mwekezaji atataka kuja kwenye nchi ambayo haina Amani,., Kwahiyo huu ni mchango mkubwa sana unaotolewa na Jeshi kwa uchumi wa nchi” Amesema Dkt Stergomena Tax
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilianzishwa rasmi septemba mwaka 1964,Na kupewa wajibu wa kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi wa mipaka, kufundisha umma shughuli za ulinzi wa Taifa, kushirikiana na mamlaka za kiraia kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa dharura, kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji mali, kushiriki ulinzi wa Amani kimataifa na kutoa huduma mbalimbali za kijamii.
Tazama mahojiano hayo kwa undani.