Aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, David Kafulila amejitokeza mbele ya waandishi wa habari na kuituhumu NEC na Msimamizi wa uchaguzi kwa kile alichodai kuwa wamenyang’anya ushindi wake.

Kafulila ambaye msimamizi wa uchaguzi alimtangaza kushika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha uchaguzi, alieleza kuwa yeye ndiye mshindi halali na kwamba amepanga kufungua kesi katika Mahakama Kuu ili mahakama hiyo itangaze matokeo halali.

“Mimi uchaguzi nimeshinda, isipokuwa nimenyang’anywa. Hii sio kuibiwa, mimi sijaibiwa, mimi nimenyang’anywa. Na ndio maana nasema hapa kwenye kesi kama hii sio kesi ya kwenda kurudia uchaguzi, ni kesi ya kuhesabu matokeo kwa sababu matokeo yapo,” alisema.

Kafulila aliwaonesha wana habari fomu alizokuwa amezibeba mkononi na kueleza kuwa ni fomu halisi alizozikusanya kwenye vituo vyote vya uchaguzi jimboni humo na kwamba zinaonesha kuwa amemshinda mpinzani wake wa Chama Cha Mapinduzi.

“Kwa hiyo hizi ni fomu za vituo vyote 182, kuna kila kituo hapa na ni fomu ambazo zina mihuri ya serikali… zina mihuri ya Tume kwenye kila kituo ziko hapa. Ukihesabu jumla ya hizi fomu nimepata kura 34,149, na Mgombea wa CCM, [Husna Mwilima] amepata kura 32982.”

David Kafulila alikuwa mbunge mtetezi wa jimbo hilo ambaye alipata umaarufu zaidi baada ya kuibua sakata la Escrow bungeni, sakata lilipelekea mawaziri wawili serikali ya awamu ya nne kujiuzulu.

 

Ushindi wa Tundu Lissu Wazua Utata
Ikulu Yakanusha Madai Ya Maalim Seif