Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris anatarajiwa kutembelea Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania mwishoni mwa Mwezi huu, Ofisi yake imetoa taarifa na kusema ujio huo ni maandalizi ya ziara ya Rais wa Marekani Joe Biden ambaye atatembelea Afrika mwishoni mwa mwaka huu.
Kamala anakuwa Kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu zaidi katika Utawala wa Biden kutembelea Afrika ambapo ziara yake inalenga kuchochea zaidi uhusiano baina ya Marekani na Mataifa ya Afrika kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi na kiusalama.
Ziara ya Harris itaanzia Ghana kisha Tanzania na atamalizia ziara yake hiyo ya Wiki nzima kwa kutembelea Zambia kabla ya kurejea Washington ambapo pamoja na mambo mengine atakutana na kufanya mazungumzo na Marais wa Nchi hizi tatu.
Miongoni mwa mambo anayotarajia kujadili na Marais wa Nchi hizi tatu ni vipaumbele vya Ukanda wa Afrika na Dunia kwa ujumla ikiwemo Demokrasia, kukua kwa uchumi, usalama wa chakula na madhara ya vita ya Urusi na Ukraine.