Aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya (ADU), Godfrey Nzowa ameeleza kuwa maisha yake ya miaka kumi katika kazi hiyo yalitengeneza maadui wengi waliosuka mpango kabambe wa kumtoa roho.

Nzowa ambaye ana historia ya kukamata watuhumiwa wengi wa dawa za kulevya pamoja dawa hizo akififisha nguvu ya biashara hiyo nchini, amesema kuwa wafanyabiashara hao walifanya kazi kubwa wakitaka awe upande wao.

Amesema kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wakimtafuta wakitaka wampe rushwa ya shilingi bilioni 3 baada ya kukamata watuhumiwa wengi wa dawa za kulevya pamoja na wale waliokuwa wapanga mikakati wakuu.

Akizungumzia namna walivyopanga kumuua, Nzowa ameeleza kuwa alikuwa amehudhuria mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi nchini Kenya, lakini alipata habari za kiintelijensia kuwa wauaji wa kukodi wamepanga kumuua atakapokuwa njiani kuelekea hotelini kwake.

“Walipanga kunikamata sehemu flani kati ya ulipokuwa ukumbi wa mikutano na hoteli niliyofikia. Mpango wao ulikuwa kunishtukiza wakati narudi hotelini,” Nzowa aliliambia The Citizen kwenye mahojiano maalum.

Alisema baada ya kutaarifiwa, alivuruga mipango yao kwa kuondoka ukumbini kabla ya muda na alitumia gari tofauti na kupita njia tofauti.

“Kulikuwa na vitisho vingi sana. Ni kwa neema ya Mungu tu niko hai leo,” alisema Nzowa.

Katika kipindi chake, ADU ilifanikiwa kukamata Kilo 1,173 za heroin na kilo 395 za Cocaine. Pia, zaidi ya watuhumiwa 2,800 walikamatwa kwa makosa ya biashara ya dawa za kulevya kati ya Januari 2009 na Disemba 2014.

Walioisaliti Simba SC Msimu Wa 2015-16 Watajwa Hadharani
Makamu wa Rais akana nukuu ya Vyombo vya habari kuhusu ‘utumbuaji majipu’