Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi awashukuru Viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo kwa kukubali kukaa pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM, ili kuendeleza dhamira ya kushirikiana na kuimarisha Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Ameyasema hayo leo alipozindua Kamati ya maridhiano kati ya CCM na ACT Wazalendo Ikulu, Zanzibar na kumshukuru Rais na Mwenyekiti CCM, Dkt Samia kwa kuridhia, kufanya vikao na Viongozi wa vyama vya siasa na kusikiliza maoni yao.
Amesema, hotuba yake aliyoitoa Mwezi Novemba Mwaka 2020 wakati anazindua Baraza la Wawakilishi kuwa dhamira yake ni kuwaunganisha wananchi wote wa Zanzibar kuwa wamoja, bila kujali rangi, asili, imani za dini au itikadi za kisiasa.
Hafla hiyo, imehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud Othman na ujumbe wake pamoja na Viongozi wa CCM wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Mjumbe wa kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa – NEC, Hemed Suleiman Abdullah na ujumbe wake.