Wakaazi wa Kanda ya Pwani wanatarajia kusahau changamoto ya maji, kufuatia hatua ya utekelezaji wa mradi wa maji safi wenye thamani ya shilingi bilioni 14 katika eneo hilo.
Mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa), utawafaidisha wakaazi wa maeneo ya Mlandizi, Chalinze na Mboga, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Aron Joseph.
Akizungumza wakati watumishi wa Mamlaka hiyo wakiongozana na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete walipoitembelea kampuni ya Mabomba ya Tanzania Steel Pipes Limited (TSP) juzi, ambayo inazalisha mabomba yatakayotumika kwenye mradi huo, Mhandisi Joseph alisema kuwa mradi huo utapita Kilometa 58 na pia itatoa maji safi kwa kiwanda cha Mboga kilichoko Mkoa wa Pwani.
“Mradi utasambaza lita milioni 9.3 kwa siku na utakuwa na uwezo wa kuishi kwa miaka 20 kulingana na jinsi ulivyoundwa. Mradi huu utafaidisha watu 120,912,” alisema Mhandisi Joseph.
Mbunge wa Chalinze, Kikwete alisema kuwa mradi huo utaondoa changamoto ya tatizo la maji na akawataka wananchi kuhakikisha wanalipia bili za maji kwa uaminifu kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutokomeza changamoto ya maji.
Mradi huo unatarajia kukamilika kwa asilimia 95 mwaka 2020, kwa mujibu wa Dawasa.