Mbunge wa Geita mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amewashauri Wakulima wa zao la Pamba wawe wavumilivu badala ya kuuza Pamba hiyo kwa walanguzi kwa bei ya chini huku Serikali ikiendelea kuwatafutia soko zuri.
Amesema kuwa Serikali ilishaahidi kuwa kama Pamba hiyo haitanunuliwa kwa bei elekezi ya kilo moja kwa shilingi 800 hadi mwezi Agosti mwaka huu basi Serikali itainunua pamba hiyo ili kuwafidia wakulima hao.
Hatua hiyo inakuja kufuatia Wafanyabiashara wengi kushindwa kununua kwa bei hiyo kutokana na bei ya soko la pamba duniani kuporomoka.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kasamwa mkoani Geita, Kanyasu amesema kuwa wafanyabiashara wameshindwa kukopa pesa benki kwa ajili ya kuinunua pamba hiyo kutokana na kukosekana kwa soko la kuiuza.
Kanyasu amesema kufuatia hali hiyo baadhi ya wakulima wamekuwa wakiuza pamba hiyo kwa shilingi 500 kwa kilo moja kwa walanguzi hali inayowadidimiza kiuchumi, ambapo ameitaja mikakati ambayo tayari Serikali imeshaichukua ikiwemo kuzungumza na Serikali ya Vietnam ambao tayari wameonyesha nia ya kununua pamba hiyo kwa Wakulima.
Aidha, amewaeleza Wakulima hao kuwa Waziri wa Kilimo anatambua tatizo hilo na ameahidi kutembelea mkoa huo kwaajili ya kuzungumza na Wakulima hao.
Kwa upande wake, Juma Kaludushi ambaye ni mkulima wa zao hilo la Pamba amesema kuwa wakulima walio wengi akiwemo na yeye wamekuwa wakiuza pamba hiyo kwa walanguzi kwa bei ya chini kwa hofu kuwa pamba hiyo itaharibika mikononi mwao.
Naye Ester Nalamo, ambaye ni Mkulima wa pamba amesema kuwa amelazimika kuuza pamba kwa bei ya chini ili aweze kuwalipia ada watoto wake kwa vile yeye hana chanzo kingine cha mapato zaidi ya kuuza pamba.